Maya naye!
S |
![]() |
“Nataka
kuiona sura yako. Ujue unaweza ukawa unafanana na Cote!” Akamuona anacheka,
akajilaza juu ya mto. “Umeota ndoto gani?” “Siwezi kuota kama sijalala!” Tunda
akamtizama vizuri. “Unawaza nini?” “Kuna kitu kinaniumiza Tunda, na siwezi ku..”
Akamuona machozi yanamtoka. “Huwezi kufanya nini?” “Maisha
niliyoishi zamani! Niliharibu sana. Sasa hivi siaminiki.” Akalalamika
kwa uchungu sana.
“Mimi sio kama wewe Tunda. Mimi nilikuwa nikitangaza
nimebadilika, nikikaa hata siku 10 haziishi, naokotwa nimelewa sehemu na
nimefanyiwa mambo mabaya.”
“Kwani ulikuwa hujui?” Ikabidi Tunda aulize. “Huwezi
amini Tunda. Hata mwanzo wa hayo madawa ulikuwa ni ushawishi tu. Nilipokataa,
ni kama wakanilazimishia tulipokuwa club. Sasa kwa kuwa walikuwa marafiki,
sikujali. Ila nikapenda. Nikaanza kutumia.” Tunda akaendelea
kumsikiliza.
“Lakini kila nilipokuwa nikijitahidi kuacha baada ya hapo ikawa
kama kunaushawishi wa lazima kutoka kwa baadhi ya marafiki zangu fulani kutaka
niendelee. Na wakafikia umbali wakinitishia nikiacha kutumia nao, wananitenga
kwenye kundi na kunidhalilisha mitandaoni.” “Maya!”
Tunda akashangaa. “Kweli Tunda. Sasa ukumbuke hapo nilishakuwa mtumiaji.
Ilikuwa hauhitajiki ushawishi mkubwa sana kunirudisha kwenye madawa. Halafu
nilikuwa peke yangu, Tunda. Net hakuwepo. Sina watu wengine isipokuwa hao
marafiki zangu. Papa na Nana ni wale watu wanaofuatana kila mahali. Huwezi
kuwatenganisha kama Nana anakuwepo nyumbani. Ila mara nyingi Nana anakuwa busy
na majukumu yake.”
“Utakuja
kumuona. Sasa hivi yupo hapa kwa sababu ulikuja mgonjwa, na umetoka kwenye
matatizo hakutaka ujisikie ni kama anakukimbia. Lakini safari na majukumu ya
Nana hayaishi. Mikutano ndani na nje ya nchi ipo mingi na mfululizo na yeye ni
kiongozi kila mahali kwa hiyo lazima kuhudhuria. Hawezi kuwa anatuma
wawakilishi kila mara!”
“Nilikuwa
nakuwa peke yangu humu ndani, Tunda. Kama nilivyokwambia Net alikuwa Tanzania. Na
wakati yupo hapa pia alikuwa mtu wa mipango. Huwezi kumkuta amekaa tu. Yaani tulikuwa tunamgombania na Vic, kupata naye muda.
Mwishoe Vic akawa anashinda, mimi naachwa peke yangu.” Tunda akaumia
sana.
“Papa
naye yupo kama Net. Tena afadhali ya Net anakuwepo nyumbani mapema kidogo
sababu yako. Sasa kama Nana anakuwa hayupo nchini, basi ujue Papa alikuwa
akirudi hapa hata saa tano usiku. Anashinda kazini tu. Alikuwa mtu wakufanya
sana kazi. Ikabidi na mimi nijifunze maisha yangu. Ndipo nikatengeneza kundi la
watu niliokuwa naweza kuwapata kila ninapo wahitaji. Kuanzia asubuhi nikiwapigia
tu simu nikiwaambia tukutane mahali, hawana shida. Nikiwa na kitu kinaniumiza,
wao ndio watu wakunifariji.”
“Kwa
hiyo hata waliponishawishi niingie kwenye madawa, nilipokataa, wakanilazimisha,
sikuweza kuwabishia. Kwanza waliniwekea kwenye kinywaji tu. Wakanirudisha hapa
nyumbani nikiwa nimelewa sana. Nilipokuja kuwauliza kesho yake, wakasema ni
cocaine, waliniwekea makusudi ili nifurahie kwa kuwa nilienda kwao nikiwa
mnyonge.” “Maya!” Tunda akazidi kushangaa.
“Kweli tena Tunda. Wakanishauri nijaribu tena nione
nitakavyojisikia. Nikakataa. Ndio wakaniambia kama nakataa faraja ya kweli,
basi nisirudi tena kuwalilia shida. Kufupisha stori, ndipo nikaanza. Madawa
yakawa kimbilio lakuondoa unyonge na kuniweka karibu na marafiki.” “Pole sana Maya.” Tunda akaumia sana.
Akahisi hakuna aliyetulia na kujua upande wa Maya wa stori.
“Hapa ndani hapafai kama upo peke yako tu. Panachosha.
Panakuwa papweke sana. Muda wote unajikuta na Carter tu na Ms Emily! Na Ms
Emily akiondoka, unabaki na Carter usiku kucha. Unamfuata Carter kila mahali
mpaka unachoka. Huwezi kuishi hivyo. Na mimi nilikuwa ndio nimepevuka. Nikawa
nawafuata na ninaogopa wasiniache. Na nafikiri na wao walijua kua nawategemea,
wakatumia upweke wangu vizuri sana.”
“Usilie sasa.” Tunda akamgusa kama kumbembeleza.
“Nilikuwa nateseka Tunda! Acha tu. Wanachukua pesa zangu.
Wanataka mimi ndio ni wanunulie kila wakati. Nikiwaambia sina hela, wakati
mwingine wananifukuza.” “Jamani
Maya!” “Kweli Tunda. Basi unarudi nyumbani unatulia
mpaka ukipata tena pesa ndio nawatafuta. Nikaendelea kuharibikiwa, hakuna
anayejua wala kujali. Mpaka waje wanione kwenye mitandao au wafuatwe na polisi
hapa kuwa labda nimekwama mahali, ndipo utawaona wote wanaacha shuguli zao na
kunijali. Hata kama Nana anakuwa mbali vipi. Akisikia tu nipo kwenye shida
anarudi siku hiyohiyo. Lakini sio kujali siku yangu inaendaje nikiwa sipo
matatizoni.” Maya akaendelea kulia taratibu.
“Niliyaharibu maisha yangu sana Tunda. Sina sifa nzuri popote na
kwa yeyote. Hata sasa hivi nikiongea kitu kwa mtu, siaminiki. Wananiona mimi
muongo tu. Ukiwasogelea karibu wale watu wamaana au vijana wa maana,
wanakukwepa au wazazi wao wanakufukuza waziwazi wanaona unataka kuwaharibia
maisha vijana wao.” Tunda
aliumia sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaona
Maya hakuwa na tofauti yeyote ile na yeye. Sema yeye alizaliwa kwenye pesa,
Tunda kwenye dhiki. Lakini ni kama walifanana kabisa. Kujikuza wenyewe kwenye
nyumba zilizojaa watu wazima na akili zao! Upweke ukawafanya wote waangukie
pabaya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Lakini Tunda, mimi nafikiri ni kama Vic anahusika.” “Kwa nini? Futa machozi uniambie ukiwa
umetulia.” Maya akajaribu kutulia akaendelea. “Sina ushahidi, lakini kila
nikifikiria, ni kama wale watu waliokuwa wananizunguka, ni kama walikuwa
wanatumwa Tunda. Kunisukumia kwa makusudi kwenye madawa. Na kila nilipokuwa
nikitaka kutoka, walikuwa wanahakikisha narudi. Tena kwa pressure kubwa kama
ambao walikuwa wanasubiriwa kutoa matokeo fulani.” “Pole sana Maya. Pole.”
“Kijana
wa mwisho niliyekuwa naye, alikuja kwangu kama ana uwezo mzuri tu. Akaniambia
mambo mengi sana. Nikamleta mpaka hapa nyumbani kwa Papa na Nana. Ikawa sasa
zamu yake yakunipeleka kwao au kwa wazazi wake. Nikaona ni kama ananizungusha
kwa hili na lile.” Akaendelea.
“Mimi
najijua kuwa nina akili sana. Hilo nalijua. Hata zakufikiria huwa najua ninazo.”
Tunda akacheka. “Kweli Tunda. Sema sikuwahi kujipa nafasi. Lakini huwa
nikidanganywa huwa najua. Naweza nikaamua kujifanya mjinga tu, lakini huwa
najua kama ninadanganywa. Na ninaweza kumsoma mtu na kumjua kwa kumsoma tu
usoni. Na tukipata hata dakika 5 za mazungumzo, ndio kabisaa. Hujifichi kwangu.”
Akaendelea.
“Akanizungusha
sana, mwishoe akaniambia atanipeleka nyumbani kwake nimpe muda.” “Sababu gani
alikupa kubwa ya kutokukupeleka kwa wazazi?” Tunda akauliza. “Alisema hayupo
kwenye maelewano mazuri na wazazi wake. Eti akasema huo ulikuwa ni mwaka wa 4,
hawaja wasiliana.” Tunda akatulia na yeye akaonyesha kutoridhika. “Siku ya
kwanza nafika nyumbani kwake, nikashangaa. Hapakuwa pakiendana na nyumba ya
mwanaume anayeishi peke yake! Pazuri sana, na pamepangiliwa vizuri kama mtu
aliyekuwa ameajiri designer apapangilie. Halafu hapakuwa na dalili kama
alishawahi hata kulala usiku uliopita! Kila kitu kipya kabisa. Nikajaribu kumuuliza
maswali kadhaa, nikajua anadanganya ila sikujua ni kwa nini.”
“Nikajiambia
pengine anafanya hivyo ili kunivutia kwa kuwa anajua mimi ni Cote. Nikawa
najaribu kumfanya atulie ili awe kama yeye. Nafikiri akaja kunipenda. Sasa
nahisi Vic anakuja hapa.” Maya akakaa vizuri.
“Siku
moja nikiwa nyumbani kwake, simu ikaita. Akaonekana kupaniki kidogo, akaomba
kwenda kuzungumza nayo nje. Nikamwambia hamna shida. Lakini tayari
nilishaingiwa na mashaka kwa jinsi alivyo paniki. Nikajiambia nilazima nijiibe
nisikilize. Hapo mapenzi yalikuwa yamekolea! Wakati
wote yule kijana alitaka aniweke mikononi. Si kwa kufanya mapenzi, ila tu
kunishika. Tunakaa hata masaa, amenikumbatia tu.” Machozi yakaanza
kumtoka tena Maya.
“Sikuwahi kupendwa vile Tunda. Sikuwahi kujisikia salama vile.
Upweke wote uliondoka. Wengi walinichezea. Na mimi nilijua kuwa nacheza tu.
Lakini yeye, alinipenda. Mapenzi yetu yalianza kukua taratibu mpaka nafikiri
hata yeye akajua mimi ni mtu wake. Akaanza kufungua moyo wake kwa ukweli. Akawa
akifufurahia kweli akiniona tofauti na zamani. Mimi mwenyewe niliona
mabadiliko.” “Mbona humtaji
jina?” “Alinidanganya Tunda. Najuaje kama hata jina
alilonipa ni lake kweli?” Akajifuta machozi.
“Usilie
sasa ili unisimulie ni kipi kinakufanya uhisi kama ni Vic.” Maya akajifuta
machozi. “Alitoka nje kwenda kuzungumza na simu. Nikajificha kusikiliza. Kitu
kikubwa nilichomsikia akiongea na huyo mtu ambaye ni kama alikuwa akimpa
maagizo na yeye kuitiki ni, ‘Hapana, sitaweza kumfanyia
hivyo, anaonekana ni mtu mzuri sana. Na amebadilika. Haonyeshi kama ni mtu hatarishi,
ambaye hata wewe atakuingilia.’ Kama anayekataa kunifanyia kitu ambacho
walikubaliana na huyo mtu.” “Maya!” Tunda akashangaa sana.
“Kweli
tena Tunda. Baada ya hapo akaonekana kupoooza sana. Ukumbuke hapo hata madawa
hatukuwa tukitumia. Nikajaribu kumuuliza ni nini? Akashindwa kabisa kuniambia,
ila ni kama akaniaga kuwa anaondoka, anaweza asirudi tena. Akawa ni kama mtu
aliyejawa na hukumu. Nafikiri ni kwa vile nilivyokuwa nimemueleza maisha
machafu niliyoishi nyuma na kumwambia nimeamua kubadilika kabisa. Sitakaa
nikarudia hata pombe. Sasa nafikiri dhamira ilikuwa ikimsuta kuja kunirudisha
kule.” “Pengine!” Tunda akaafiki.
“Kosa
nililofanya, nikumlilia. Nilikuwa nasikia kuchanganyikiwa, ile kuhisi kama
atakuja kuondoka aniache tena! Narudi kwa nani! Naishije bila yeye! Tulikuja kuwa
tukipatana sana. Aliishi na mimi akijua ni nini anifanyie na kwa wakati gani.
Hatukuwa tukibishana. Yaani alikuwa akinipenda na kunidekeza. Simu kila wakati
kitu ambacho nahisi aliambiwa kuwa mimi ni mpweke, nahitaji mtu maishani.”
“Sasa
nahisi aliingia kwenye mahusiano ya wizi akiwa amefundishwa ni nini anifanyie
kwa vile huyo mtu alivyokuwa akinifahamu. Nakwambia alikuwa mtu sahihi. Hakosei
kwa lolote. Kwa hiyo ikatusaidia kujenga penzi la kweli kwa haraka, yeye
mwenyewe akanasa vibaya sana.” “Na wewe Maya unapendeka.” Maya akacheka kwa
unyonge.
“Turudi
kwenye kutaka kuondoka kwake.” “Ehe!” “Basi. Nilikuwa sipo tayari kumpoteza.
Hapo ukumbuke nilikuwa nimeacha madawa, na pombe. Sina rafiki. Wale rafiki wote
wa zamani nilishachana nao. Na wao kama ajabu hivi, wakaacha kabisa kunitafuta.
Na mimi nikashukuru Mungu. Nikawa napata muda na Andy wangu.” Tunda akacheka
baada ya Maya kuropoka.
Maya
akagundua ameropoka jina, akacheka kwa unyonge akainama kwa muda kisha
akaendelea. “Na kipindi hicho ndio Papa naye alikuwa amezidiwa. Akili za Nana
zipo kwa Papa tu. Net yupo Tanzania. Kwa hiyo yeye ndio alikuwa amebaki
kimbilio langu. Papa akizidiwa, basi yeye anakuwepo kunibembeleza na kuwa na
mimi.”
“Nikamlilia
sana na kumsihi sana asiondoke tufanye kila namna tuwe wote. Nikamwambia kama inamlazimu
kuondoka, basi tuondoke wote. Asiniache. Aondoke na mimi tukaanze naye maisha.
Nikashangaa analia. Alilia Andy! Mpaka nikashangaa. Aliniambia wazi kabisa, hajawahi
kupata upendo mkubwa wa kiasi kile, na anaumia sana. Nikamuuliza unaumia nini!
Sasa mimi mawazo yakawa kuwa anaumia kwa kutengana! Nikamwambia kama shida ni pesa,
mimi nitamsaidia mpaka atakapopata kazi ya maana.” “Kwani hakuwa na kazi?”
Tunda akauliza.
“Ndio
kilichokuwa kikinishangaza Tunda. Alikuwa anaishi pazuri. Gari nzuri. Kuvaa
vizuri, lakini hana kazi yakueleweka. Ukimuuliza unafanya kazi gani au biashara
gani, hana jibu la maana. Mara aniambie anauza hisa online. Na kweli, biashara
ya hisa huwa ina pesa kama ukiipatia. Lakini Tunda, ilikuwa hata ukimuuliza
tena juu ya hiyo biashara napo akawa hana majibu ya kueleweka. Ni kama mtu
aliyeambiwa aniambie tu hivyo ili kuniridhisha au kunitoa wasiwasi wa kwa nini
yupo tu siku nzima. Maana alikuwa na muda wakutosha sana na mimi tofauti na
mafanikio yake.” “Unamaanisha nini?”
Akauliza Tunda.
“Wote
tunajua utajiri una gharama Tunda. Wewe si unamuona Net? Japokuwa anakupenda na
angetamani kuwa hapa na wewe, hawezi. Kazi zinamfunga sana. Na ndio maana
wakati wote anashukuru kwa kumvumilia. Sijui kama unanielewa?” “Hapo nakuelewa.”
Tunda akakubali. “Huwezi kuwa na pesa nyingi kama huzitafuti kwa bidii! Labda
uwe unapewa kama Vic anavyotunzwa na wazazi wake tu.” “Kwani hafanyi kazi?”
“Hana anachofanya. Ila amesoma. Ukimuona na kumsikiliza, ana mipango mingi
mizuri, lakini hajui kuitekeleza.”
“Anajitangazia
kuwa anafanya kazi kwenye kampuni ya wazazi wake, lakini kutwa yupo mtaani na
mitandaoni akijinadi kwa hili na lile. Kila kitu kwake ni tukio la mtandaoni.
Maisha yake yote yapo mtandaoni. Kuanzia asubuhi mpaka usiku. Na watu
wanamfuatilia kwa sababu ya vitu vizuri anavyovionyesha. Nitakuja kukuonyesha.”
“Wala sitaki. Sina huo muda mimi.” Hilo
likamgusa sana Maya.
“Na
mimi nitakuiga Tunda.” Wakacheka. “Sasa ndio turudi kwa Andy, akaonyesha
utajiri mkubwa, lakini yupo tu. Nafikiri ndio maana akaja au akapewa sasa hilo
wazo la kunidanganya kuwa anaingiza pesa popote alipo, na muda wowote. Na si
unajua ni biashara ambayo ukielewa huhitaji kuwa mtandaoni kila wakati!
Ukishauza asubuhi au usiku, basi. Nikujua wakati gani ni mwafaka wakuingia
sokoni, ukiuza pesa yako inaingia bila shida. Lakini haya ninayokwambia hata
yeye mwenyewe hakuwa akiyajua kwa undani hivi kama mimi ambaye hata hiyo biashara
sifanyi.” “Wewe umejuaje?” Maya akacheka.
“Unafikiri
kwa nini kina Cote wamedumu na utajiri kwa miaka mingi? Ni moja ya kitega
uchumi cha kina Cote. Mumeo ndio bingwa wa hiyo. Alitoa kwa babu. Na wazazi
wake Vic pia walirithi kutoka kwa wazazi wao ambao walikuwa marafiki wakaribu
sana wa Papa na Nana. Ndio maana nahisi alikuwa ni mtu wa Vic. Aliyemtafuta
maalumu kwa kazi moja tu ya kuniangamiza.” “Jamani!” “Kwa kuwa nilitulia sana
Tunda. Sana. Na yeye akaja kama kijana mtulivu na wamaana. Mzuri. Ungetamani
anioe tu. Kwa hiyo moja kwa moja mimi ndio ningekuwa mrithi wa Nana, kitu
ambacho Vic asingekubali kabisa.”
“Anyway,
nikaanza kumuona anabadilika. Hana raha. Kama anayetaka kuniambia kitu lakini
hawezi. Ndipo akaanza ulevi sasa kama ambaye yupo na jambo zito linalomfunga.
Pombe ikawa ndio silaha ya kunikwepa. Hata mchana unamkuta amelewa. Ukumbuke
hapo mimi nilikuwa sitakiwi kuonja hata wine. Kileo chochote kile siruhusiwi
hata kukiweka mdomoni.”
“Mambo
yakabadilika. Ukimtafuta, unamkuta club amelewa na hataki kuondoka. Kumbuka
nilikuwa nampenda Tunda. Sikuwa naweza kumuacha kwenye ile hali pale.
Akionekana ana jambo linalomuumiza, wakati mimi ndio alikuwa faraja yangu! Nikawa
nakaa naye huku nikimsihi nimrudishe nyumbani asiendeshe akiwa amelewa.
Mwanzoni nikafanikiwa kuwa nikimrudisha akiwa amelewa, mimi sinywi. Namrudisha
mpaka kwake. Nikihakikisha amelala, ndio na mimi naondoka.”
“Kukutana
kwetu sasa kukageuka. Sio tena nyumbani kwake kwenye makochi tukikumbatiana. Andy
akaanza maisha yakuwa club. Usiku kucha na hataki kuongea. Ukimuuliza
anakwambia kila kitu kitakuwa sawa tu. Lakini hapakuwa na mabadiliko. Haikuchukua
muda na mimi nikaanza kunywa kidogo wakati nikimsubiria yeye turudi nyumbani.
Nikaanza tena pombe, napo haikuchukua muda, nikarudia madawa kabisa.” “Sas..”
Tunda akataka kuuliza.
“Subiri
kwanza Tunda. Wewe jiulize tu. Tulikuwa mimi na yule kijana tu. Nani alikuwa na
uwezo wa kuingia chumbani kwake, bafuni, kutufuata kwenye gari na kutupiga
picha na kutuchukua video?” “Lakini kweli! Labda rafiki zake?” Tunda akatoa
wazo.
“Na
mimi ningedhani hivyo Tunda. Andy hakuwa mzawa wa Norfolk. Alikuwa mgeni
kabisa. Watu walikuwa hawamfahamu. Mimi aliniambia amehamia hapa makusudi
kuanza maisha mapya. Hakuwa na rafiki na aliniambia hakuwa akimfahamu mtu
yeyote kwenye huu mji ila mimi tu. Na aligoma kabisa kutengeneza marafiki.”
“Maya!” Tunda akazidi kushangaa.
“Nikikwambia
alikuwa na muda na mimi, niamini alikuwa na muda na mimi. Sikuwahi hata kumuona
akisalimiana na mtu. Akili na mawazo yake yalikuwa
kwangu tu. Unafikiri kwa nini nilichanganyikiwa aliponiambia anaondoka au kwa
nini nilimleta yeye kwa Papa na si wanaume wengine?” Maya akauliza huku
machozi yakimtoka.
“Kwa kuwa aliniaminisha mimi ndio mtu wa pekee na kitu cha
thamani kilichotokea kwenye maisha yake bila hata ya yeye mwenyewe kutarajia!
Andy alinionyesha mapenzi Tunda, sitakaa nikasahau. Ndio maana nikimfikiria
sasa hivi ndio naona kuna kitu hakikuwa sawa. Kwa kuwa alianza kiusanii kabisa,
lakini akaja kukolea haswa.” Akajifuta
machozi.
“Tulipokuwa
tumefika na Andy, ni ilikuwa heri umfanyie yeye kitu ila si mimi. Alikuwa
tayari kunifanyia kila kitu ili tu kunifurahisha. Na si ya kutumwa. Ungemuona
akifanya kutoka moyoni. Wengi waliokuwa wakinifanyia uchafu na kunichukua video
na kunipiga picha walifanya kwa sababu
maalumu. Wengine ilikuwa kama ulinzi wa kuniweka kwao. Ili nisiwaache.
Niendelee kuwa nao tu. Na wengine pesa. Kwa hiyo ikitokea kama mimi siwapi pesa
wanazotaka, wanaziuza zile picha au video zangu za ngono magazetini au kwa watu
kama Vic. Na walikuwa wakiziuza kwa pesa nyingi sana.” “Maya!”
“Kweli
Tunda! Nani asiyependa kununu gazeti lenye habari nzito za kina Cote? Kwanza
walikuwa wakizitafuta picha zangu za ngono ili kuuza magazeti yao. Na kwa upande wa mahusiano, ilikuwa nikiwaacha,
wakiomba niwarudie, nikikataa hapo ndipo walikuwa wananitoa mitandaoni wakinichafua
kama kunikomoa” “Pole Maya.” Tunda akamuhurumia.
“Lakini
yeye Andy ilikuwa tofauti. Siku ya kwanza nimelewa Club, alihangaika sana
kunitoa pale bila watu kuniona na kunipiga picha. Alimuomba baunsa wa pale
wanitoe mlango wa nyuma. Na akamlipa pesa nyingi tu kuhakikisha sionekaniki na
mtu. Akanibeba mpaka kwake. Maana aliniacha mezani akaenda kucheza draft.
Akapata mtu wakushindana naye, mimi huku nyuma nikaanza kunywa. Kuja kurudi
kuniangalia, ndio akanikuta nimelewa. Aliumia sana.”
“Kesho
yake akaniomba msamaha wakunirudisha club, na akaniapia hatutarudi tena club.
Na akaniambia atabadilika, na atanisaidia niache pombe. Tulirudia maisha ya
kukaa ndani tu. Sasa kwa shida yote ile aliyofanya, kwa nini anichafue tena!?”
“Kweli hapo kuna utata!” Hata Tunda akaafikiana naye. “Halafu Tunda, turudi kwenye
maisha yake na ile nyumba. Unakumbuka nilikwambia siku ya kwanza tulifika vitu
vingi kwenye ile nyumba niligundua ni vipya!” “Nakumbuka.” Tunda akaitika.
“Halafu
Tunda, nyumba aliyokuwa akiishi mtu kwa muda mrefu au kama ni yake, inajulikana
tu. Kuna milango alikuwa hawezi hata kufungua. Hilo moja. Halafu mtu tajiri, au
aliyezaliwa kwenye utajiri, kuna vitu ambavyo anajua tu. Yaani hawezi
kubabaika. Ule ustaarabu unakuwa sio wakujifunza, amezaliwa kwenye hayo maisha
anajua. Lakini yule kijana alikuwa mshamba kabisa. Vitu vingine mpaka nilikuwa
nikimshangaa vile ambavyo asivyo na uelewa navyo au anavyobabaishwa navyo!” “Inakuwa
ni kama mtu aliyehamishiwa sehemu au kwenye maisha mageni kabisa kwake?” Tunda akamuuliza akiwa kama amepata picha ya
nini anachomaanisha Maya. “Hapo umenielewa Tunda. Inakuwa ni kama alilipwa
kuishi yale maisha. Wakati mwingine alikuwa mpaka anachanganywa na aina ya saa
mpya ambayo anakuwa amevaa yeye mwenyewe akiniambia amejinunulia!” Tunda
akacheka.
“Sikudanganyi
Tunda!” “Labda alikuwa analetewa na huyo Vic.” “Sasa hapo ndio umekuja kwenye kile
ninachotaka kukuhakikishia kuwa ni Vic tu. Yule kijana alikuwa akivaa kutokana
na pesa ya Vic, ambayo ni kiwango cha juu sana. Hapo Vic alifanya bila
kufikiria. Kwa kuwa Vic ni wa viwango vya juu sana. Hajui vitu vyenye thamani
ya chini na kwa kuwa hana akili ya kufikiria kabisa. Vic ni mjinga haswa. Sasa
ndio maana alishindwa hata kutafuta vitu angalau vya daraja la pili tu,
akashindwa kufikiria hapo. Akawa anamnunulia vitu vya thamani sana na kumpa
akidhani na yeye Andy atafikiria kama yeye, kumbe Andy hajawahi hata kufikiria
kuvaa saa za mapesa yote hayo. Ndio maana alikuwa yeye mwenyewe Andy anashituka.
Kwa kuwa hajazoea.” Tunda akazidi kucheka.
“Sasa
nahisi aliponipenda, pale mwanzo kabisa nilipomsikia akiongea na simu, nahisi
alikuwa akimkatalia Vic asinifanyie mambo mabaya. Ndio Vic akamshawishi labda
kwa kumtisha.” Maya akafikiria kidogo. “Unajua kuna kitu kimoja kikubwa sana
ambacho Vic amenipita nacho, Tunda?” “Nini?” “Kwa kina Vic, Vic ni kama mboni
ya jicho. Akili na mawazo ya wazazi wake Vic, vipo kwa Vic wakati wote.
Anajaliwa, na kulindwa sana na wazazi wake. Mtu kama huyo hawezi kuangamia kirahisi.
Hata katika ujinga wake, mama yake anamuunga mkono
na kumsaidia ili afanikiwe. Wakati mimi ni kinyume.” Akaanza kulia tena.
“Usilie
Maya wangu. Sasa hivi mimi nipo.” “Lakini
imeniharibia Tunda. Imeniharibia sana. Siaminiki!” “Upande gani? Mbona
sasa hivi unakazi nzuri! Nana amekuamini!” “Kumbuka mimi ni Cote, Tunda.
Sijawahi kuwa na shida na pesa. Sasa hivi nafanya kazi ili tu kuonyesha uma
ninaweza na kuwaaminisha nimebadilika. Lakini sina shida mimi, Tunda. Naweza
nikaishi maisha yangu yote bila kufanya kazi na nikawa sawa tu.” Maya
akaendelea.
“Papa
alipofariki, japokuwa Net ni mrithi wa Cote, binafsi nina share zangu. Naweza
nikaamuru pesa iwe inaingia tu kila week kwenye akaunti yangu, nisifanye kazi na
nikaishi vizuri tu.” “Na madeni yako?” Maya akacheka na kuanza kulia tena. “Nakaribia kumaliza Tunda. Naomba usinikumbushe! Nilikuwa
nadaiwa mamilioni ya pesa.” “Haya nyamaza basi tuzungumze.” Kakanyamaza.
“Sasa
kama Net na Nana wanakuamini, unataka nani akuamini?” “Nikikwambia utamwambia
Net. Halafu Net anaweza kuchanganyikiwa kabisa.” Tunda akakunja uso na kukaa. “Ni
nani?” Maya akamwangalia kwa muda. “Mmmmhh! Nooooooo! No no nooo.” Akakataa
mpaka akasimama kabisa. Tunda akaanza kucheka. “Ni nani?” “Sikwambii ila ujue
historia yangu ya zamani inaniharibia sana Tunda. Siaminiki.” Tunda akafikiria
kwa haraka.
“Nisikilize
Maya. Mungu amekupa nafasi ya pili, itumie vizuri.” “Mimi ni tofauti na wewe
Tunda. Nilishapewa nafazi zaidi ya 5, na zote nikaziharibu vibaya sana. Nani
ataamini sasa hivi nitabadilika? Wanajua mimi ni
bomu tu, ambalo wakati wowote naweza kulipuka.”
“Nisikilize Maya. Acha
kulia na urudi hapa ukae.” Akarudi kukaa. “Wape watu muda na sababu ya
kukuamini. Na wewe kusudia kutorudi huko tena.” “Nimekusudia
Tunda, lakini naogopa. Sijui litakalonipata tena.” Akaanza kulia tena. “Nilipomaliza chuo, nilikusudia kubadilika. Huwezi amini,
mimi Maya, nilitulia mpaka nikafikia kipindi cha kutaka kuolewa niwe mke wa
mtu.” Tunda akaanza kucheka. “Usinicheke
bwana!” Kakaendelea kulia.
“Mimi
sijui kwa nini! Nakuamini Maya. Naamini ukipata mwanaume mtulivu na akakupenda
kwa dhati vile ulivyo, unaweza kabisa kuwa mke mzuri na ukaweza kumfanya
mwanaume kuwa na utulivu.” “Kweli Tunda?” “Kabisa. Unaweza. Umejawa upendo na
ni mkarimu sana. Na mimi nipo na wewe Maya. Siwezi kuruhusu Vic akarudia
michezo yake, kama anahusika. Na siwezi kukuacha mpweke.” Akamuona anacheka
huku anafuta machozi.
“Usilie.
Ukumbuke mimi nipo na wewe katika kila jambo. Ni vile sasa hivi bado ni mdhaifu
tu na ninamuhofia Cote. Sitaki chochote kitokee. Lakini nikijifungua salama,
nimemwambia hata Net. Tutakuwa na sisi na siku yetu yakutoka.” “Kweli Tunda?” “Kabisa! Hee! Wewe si mfungwa,
na ninaamini kuna njia nyingi tu na sehemu nyingi tu unaweza kufurahia mbali na
club na hao marafiki wanaotaka kukutumia tu. Wajinga kabisa.” Tunda akachukia
kabisa. Alikumbushwa na yeye vile watu walivyokuwa wakimtumia kwa manufaa yao.
“Niombee
Mungu nijifungue salama na Cote akue salama. Tutapanga. Na tutakuwa tunakwenda
sehemu nzuri, sahihi ili tu kufurahia. Na ninakuahidi kukulinda. Usiogope kuanguka
tena. Ila ujifunze kuomba kama kaka yako. Net anaomba ile ya kupiga magoti.
Wewe unakuwa na muda wa kumuomba Mungu?” “Hata kidogo. Nikiamka tu nakimbilia
kuangalia saa kujua kama Net amenipisha hapa, na mimi nije.” Tunda akaanza kucheka.
Akazungumza
naye kwa kumfariji mpaka akaweza kwenda kazini akiwa amechangamka, japo hakuwa
amemwambia ni nini kinamsumbua! Na Tunda akapata shauku yakutaka kujua “Ni
nani anayesumbua kichwa cha Maya, akimtaka amwamini lakini ameshindwa!” Tunda
akabakiwa na hilo swali baada ya kuunganisha malalamiko yote ya Maya, akajua
kuna mtu ameanza kumsumbua kichwa.
“Alirudia
vipi madawa!” Hilo nalo
likaibuka kichwani kwa Tunda. Maya aliishia kumwambia Andy alimuahidi
hawatarudi tena Club na wala kunywa pombe. “Nini kilitokea tena? Ni kweli
Andy alionyesha kumlinda Maya. Nani alikuwa na uwezo wa kuingia ndani kwa Andy
na kuwapiga picha wakiwa wamelewa? Ni kweli Vic anakihitaji hiki cheo cha bibi
Cote! Kama alikwenda umbali wote huo wa kumuharibia Maya kiasi hicho, mimi je?”
Tunda akabakiwa na hayo maswali akiyatafakari baada ya Maya kuondoka. Akaamua
kuyapa muda yaje yajijibu au akipata tena muda kama wa siku hiyo na Maya basi
amuulize ambayo yatakuwa hayajajibika.
Mkasa wa Kwenye Kutafuta Chakula Cha Harusi.
M |
aya alikwenda kazini
asubuhi kama kawaida na bibi yao na Net ambaye alishaondoka mapema sana
alfajiri ya siku hiyo. Carter alishaandaa usafiri wa kumpeleka Tunda kwenye
hayo mahoteli ambako ilikuwa wakutane na Gino pia hukohuko ili amsaidie kuonja
hivyo vyakula kisha amsaidie kufanya maamuzi.
Tunda
alipofika kwenye hoteli ya kwanza, akakuta mpaka Net anamsubiria. Akafurahi
sana kuwaona pale. Akaanza kucheka. “Sikutegemea kuwakuta hapa na nyinyi!”
Akimaanisha bibi Cote na Net. Akamkumbatia Maya. Maya akamtania kidogo,
akamsogelea bibi Cote, akamtania kidogo, ndipo akamsogelea Net, akambusu. “Nimeona tu nije. Vipi wewe na Cote?” “Tupo
sawa. Nilikuwa na watu wa nguo nyumbani, karibu siku nzima. Anasema itabidi
kuwa makini na vipimo vya nguo. Ameangalia ukuaji wake kwa kila week, anasema
ni mtoto anayekuwa haraka. Inabidi aongeze umakini kwenye hilo gauni. Tunaweza
kufika siku yenyewe, gauni likawa halitoshi. Mwanao amekazana kukua kama uyoga!”
Wote wakacheka. Net akapiga magoti na kumbusu tumbo.
“Asante
Nana kwa kuja. Nimefurahi!” Tunda akamshukuru bibi Cote na sura iliyojaa furaha
tele. Bibi Cote akacheka. “Unafikiri kuna ambaye angejali chakula ambacho
ungechagua?” Tunda akacheka. “Lakini kwa sasa mimi sio mtu mzuri wa kutoa
uamuzi mzuri juu ya chakula. Bado kuna vyakula kama samaki siwezi kuvila kabisa.
Sikutaka kuwanywesha wote uji wa ulezi.” Wote wakacheka. Bado Net alikuwa
amepiga goti moja huku akimpapasa Tunda. “Mimi ningekunywa tu.” Maya akadakia,
wote wakacheka.
Net
akasimama na kuangalia saa. “Gino yuko wapi?” “Amenipigia simu wakati tupo
njiani. Ameniambia atachelewa dakika kama 5 zaidi.” Akamuona Net amekunja uso,
akaangalia tena saa. “Kama 5 au dakika 5? Hatuwezi kumsubiria yeye. Tuna..”
Tunda akamshika mkono taratibu maana alishaanza kugomba kwa sauti. Net
akamwangalia na kutulia kidogo.
“Hatuwezi
kumsubiria, Tunda!” “Naomba tumpe hizo dakika 5.” Net akaangalia saa. “Pole na
kazi.” Ikabidi amtoe akili na macho pale kwenye saa. “Asante Tunda. Lakini Gino
anatakiwa awe akisema sawa kwa jambo awe amezingatia muda. Kama anashindwa au
anakuwa na majukumu mengine, anasema tuweke muda mwingine. Inakuwa ni kama sisi
hatuna kitu cha muhimu chakufanya, yeye ndio anakuwa na majukumu muhimu zaidi
yetu! Tunaacha shuguli, wote tupo hapa. Kumsubiri yeye!” Net aliongea kwa
ukali.
Akatoka
muhudumu wa hapo, akawasogelea kina Cote
pale walipokuwa wamesimama akiwa na tabasamu la heshima. “Bado mnasubiriana?” Akauliza
kiustarabu sana. “Call Gino. Now!” Akamgeukia kijana aliyekuwa amesimama
pembeni kama mlinzi/bodyguard. Mbali kidogo na wao. Net akampa hiyo amri akiwa
amekasirika kabisa.
“Naomba niangalie
Net.” Tunda akamuita kwa upole. Net akamgeukia. “Naomba tufanye hivi, kwa kuwa
Gino aliniomba, nikamruhusu. Na kwa kuwa sisi tumeshafika hapa, nashauri twende
tukaanze sisi kuonja hicho chakula. Nitawaambia wamuwekee Gino chakwake. Kisha
twende kwenye hoteli ya pili. Tutafanya hivyo hivyo. Kesho nitawapigia simu
kutoa maamuzi ya chakula kipi tutataka kwenye harusi yetu baada ya sisi wote
kuonja na kuchagua. Ni sawa?” Tunda akatoa ushauri akiwa ametulia na sauti
iliyotulia ili kutuliza ile hali ya wasiwasi pale.
“Lakini
hii ni zaidi ya dakika tano sasa!” Tunda akamshika mkono kama kumtaka atulie.
“Pole na samahani mpenzi wangu. Naona sisi tuanze ili asiwacheleweshe zaidi.
Kwani unarudi kazini?” “Hapana. Tunarudi wote nyumbani.” Tunda akamgeukia bibi Cote. “Samahani Nana.”
“Gino anajua hakupaswa kuchelewa hata kwako. Anafanya hivi, akijua ni wewe tu
na Maya, sidhani kama anajua kama Net na mimi tutakuwepo hapa.” Bibi Cote
akaongeza. “Pole Nana na samahani.” Tunda akaendelea kuomba msamaha ili
kutulie.
“Naona
tufuate ushauri wako tu. Hatuwezi sisi ndio tukawa tukimsubiri Gino hapa! Wote
tutaonekana hovyo.” Walishangaa Maya amenyamaza kimya hata hajaongeza neno.
“Sawa Nana. Twendeni.” Tunda akamwambia yule muhudumu, wapo tayari, akaongoza
njia. Tunda na Net wakamfuata nyuma. Net akamvuta karibu, akamuwekea mkono begani
akambusu. “Umekuwa na siku ngumu?” Tunda akauliza kwa upendo tu. Net akafikiria
kidogo.
Akaanza
tena kama ambaye alikatishwa kutoa dukuduku lake. “Sipendi watu wasio heshimu
muda, Tunda. Na kila anayefanya kazi na mimi analijua hilo. Kama alivyosema Nana,
Gino hakutegemea sisi kuwepo. Ndio maana nimekasirika. Lakini sio kazini.
Kazini pako sawa.” Net akaendelea kugomba, Tunda akanyamaza kabisa, hakujibu
tena kitu. Wakaendelea kuelekea kule walipoelekezwa kuingia ili waletewe hicho
chakula.
Lakini
tayari mudi ya Tunda na yeye ikawa imeshabadilika. Akajikuta hatamani kabisa
kuwepo pale tena. Akabadilika mpaka usoni. Walipelekwa kwenye hicho chumba
walichoandaliwa vizuri sana. Kwa kuwa walikuwa ni kina Cote, kila kitu kikawa
tofauti na huduma pia. Ulinzi ukawekwa mpaka jikoni. Chakula kikaonjwa na
kusimamiwa wakati kinapelekwa mezani walipokuwepo.
Tunda
na Maya wakawa kimya. Tunda akaendelea kupapasa tumbo lake taratibu akiwa
amejiinamia. Maya macho kwenye simu yake. Wakabaki Net na bibi yake wamekaa
kimya wakiangaliana. Pakatulia kwa muda. Wakaingia wahudumu na kuanza kuwahudumia.
Tunda kimya. Zilishapita dakika 15. Akamuona Net anaangalia tena saa yake ya
mkononi, lakini akanyamaza. Na yeye akanyamaza. Aliyetumuita kumpigia Gino
alishajibu kuwa Gino hakupokea simu.
Wakati
wanakula Gino akaingia pale kwenye kile chumba kama aliyekuwa anakimbia.
Alishituka, akakaribia kama kurudi alikotoka. Wote wakanyanyua uso kumtizama.
Gino alibaki amesimama palepale mlangoni asijue aseme nini. Tunda akarudisha
uso wake kwenye sahani, kimya. Maya akamtizama kaka yake na bibi yake, na yeye
akainamia sahani yake.
“Nilijua
habari ya kuja hapa, nikiwa nimeshakubali kazi ya watu. Lakini Mrs. Cote
aliponiomba nije hapa ili nimsaidie kufanya maamuzi, nilimweleza kila kitu.
Kuwa nitakuwa na kazi kwa muda huo. Ila nikamwambia ninaweza kuja kwa kuchelewa
kidogo kama itakuwa sawa. Akakubali kwa makubaliano ya hata nikichelewa ni
sawa, ila tu nije nijaribu chakula, halafu tutaamua pamoja hata kesho. Sikujua
kama...” Gino akasita. Maana alianza
kujieleza bila hata kuulizwa. “Samahanini sana.” Mwishoe Gino akaona aombe tu
msamaha. Kimya. Net na bibi yake wakainamia sahani zao na wao kuendelea kula
bila hata kumjibu.
Gino
akabaki amesimama akiwa ameshakuwa mwekundu haswa kwa hofu. “Njoo ukae hapa.”
Ikabidi Maya amkaribishe tu, maana aliachwa akiwa amesimama. Gino akavuta kiti
na kukaa kwa tahadhari na hofu pembeni ya Tunda. Kwa hiyo akawa katikati ya
Tunda na Maya. “Samahani sana Tunda.” Akamnong’oneza Tunda, lakini walisikia.
Tunda akanyanyua kichwa akamtizama kwa tabasamu. “Ulimaliza kazi yako lakini?”
Akamuuliza taratibu tu. “Yeah. Thanks.” Gino akajibu, muhudumu akaanza
kumuhudumia na yeye.
Kilipoletwa
chakula cha aina ya baharini, Tunda akaomba yeye asipewe. Akamnong’oneza Net.
“Nitarudi baada ya muda mfupi.” “Okay. Unataka nikusindikize?” “Hapana.
Nitakuwa sawa tu, asante.” Tunda akatoka akaenda kukaa chooni kwa muda.
Alijaribu kutulia lakini akajikuta kitu kimemkaba kooni, anashindwa hata
kutulia. Hakujua kama ni hasira au nini! Alitamani kama kuondoka kabisa pale,
lakini akakukumbuka yeye ndio mwenye hiyo shuguli nzima ya kuchagua vyakula.
Hawezi kuzira.
Gafla
akahisi uchovu mwili mzima, anatamani kama alale pale. Hamu ya kila kitu
ikamuisha. Ule mukari wa sherehe ukakata gafla, akaanza kuona anajisumbua tu.
Harusi tena ya nini! Akakumbuka walishafunga ndoa Tanzania. Sasa usumbufu wote
huo ni wa nini! Akaanza kujiuliza Tunda. Alikaa hapo chooni, mwishoe akaamua
kutoka asije akachelewa na yeye.
Akatoka
kwa kujivuta wazi alionekana ule uchangamfu aliokuja nao umepotea kabisa. Akawa
anajivuta taratibu kutoka, akamkuta Net akimfuata. “Are you okay!?” “Yeah. Nipo
sawa.” Akajibu Tunda na kumuonyesha warudi wakamalize. Akampita kidogo. “Subiri
kwanza Tunda.” Tunda akageuka. “Mbona unaondoka wakati nimekufuata wewe!?”
“Sikujua kama umenifuata mimi. Nilijua na wewe unaelekea restroom. Na pia
nilikuwa naharakisha, sikutaka kuendelea kuwachelewesha zaidi, ndio maana
nilikuwa nikiwahi kurudi ndani nikihisi mtakuwa mmeshamaliza vyakula vya
baharini. Sitaki kujichefua.” Tunda akajibu taratibu tu.
“Umependa
mlo wa kwanza?” Net akauliza. “Siyo mbaya.” Akajibu na kutulia. Kimya wakabaki
wakiangaliana. “Nisawa nikirudi kule? Nataka nimalize hili zoezi la chakula,
nikapumzike. Najihisi nimechoka sana.” “Pole, Carter aliniambia ulikuwa na
wageni karibu siku nzima na fundi wa gauni naye akachukua muda mrefu. Ndio
maana niliona tuwahi ukapumzike.” Tunda kimya. “Basi twende.” Tunda akageuka
kuondoka bila kuongeza neno wala tabasamu. Ule uchangamfu ulimwisha kabisa usoni.
Sio kama alivyokuja na tabasamu na cheko juu. Net akamfuata nyuma, wakarudi
kule walipokuwa wakila wengine.
Walimaliza
pale, wakaamua kwenda hoteli ya pili. “Umekuja na usafiri Gino?” Tunda
akamuuliza taratibu wakati wanatoka pale. Gino akababaika kidogo. “Tunaweza
kuongozana tu.” Tunda akamkaribisha kwenye gari iliyomleta yeye. “Asante.” Moja
kwa moja Gino akakubali kwa kushukuru. Ndipo akajua hakuwa na usafiri. Bibi
cote alikuwa na ulinzi wake na gari aliyokuwa akiendeshwa, alishaondoka na
Maya.
“Nilifikiri
tutaongozana!” Akaongea Net kwa
kulalamika kidogo ila kwa lugha ya kiswahili. “Nilikuja na dereva. Unafikiri
nimruhusu arudi nyumbani?” Tunda akauliza kiustarabu tu. “Utakavyoamua wewe.
Lakini mimi nipo hapa kwa ajili yako. Na tukimaliza tunarudi wote nyumbani.”
“Basi ngoja nimruhusu arudi nyumbani.” Tunda akataka kuondoka kumfuata dereva
nje alipokuwa akimsubiri.
“Atampeleka Gino na kumshusha anapotaka. Leo
usiku hapatapikwa nyumbani. Si Gino amekwambia?” “Ndiyo.” Wakatoka nje ya hiyo
hoteli. Gari ya Net ikaletwa na muhudumu wa pale wa Valet, na dereva wa Tunda
akasogeza gari baada yakumuona Tunda. Net akamfungulia Tunda mlango kwenye gari
yake, akapanda, yeye akaenda kuzungumza na dereva huku Gino akimfuata nyuma.
Baada
ya kuweka mambo sawa, akamuona Net anarudi. Alishavuta kiti nyuma na kujilaza
kabisa. Akatulia, Net akaondoa gari. Kimya kwa muda. “Kesho ndio siku ya keki,
si ndiyo?” Net ni kama akapata chakuvunja ukimya. “Ndiyo.” Tunda akajibu
taratibu tu, tena kwa ufupi. Pakatulia. Tunda akajivuta zaidi kama anayemtaka
asimuongeleshe zaidi. Net naye akanyamaza.
Walifika
hoteli ya pili, walimkuta Gino alishafika. Hata hawakujua walifanyaje kufika
kwa haraka vile. Kijana alikuja kuchukua gari ya Net mara tu walipofika karibu
kabisa kwenye mlango hotelini. Net akaenda kumfungulia Tunda mlango. Akatoka
kama amelazimishwa. Hata hakumwangalia Net, akamsogelea Gino. “Vipi kile
chakula cha kwanza?” Tunda akamuuliza mara alipomfikia Gino wakati anamfungulia
mlango wa kioo wa pili wakuingia ndani. “Kawaida. Tusubiri na cha hapa tuone.”
Gino akajibu. Akasubiri Net aingie ndipo na yeye akafuata nyuma. Walimkuta bibi
Cote na Maya walishafika.
Net
akaangalia muda, waliwahi kama dakika 3. Muhudumu akawasogelea pale walipokuwa
wamesimama. Wakasalimiana. “Sisi tupo tayari wakati wowote mtakapokuwa tayari. Maana
Mrs Cote alitupa window ya nusu saa zaidi, lakini sisi tupo tayari hata sasa.
Na kama mnahitaji kusubiriana, tunaweza kuwaonyesha sehemu ya kukaa.”
Akawaambia yule muhudumu na tabasamu lililojaa heshima usoni. Net akamgeukia
Tunda kama anayemuomba muongozo Tunda. “Nafikiri tupo tayari.” Tunda akajibu taratibu
tu. Wakaelekezwa sehemu ya kwenda.
Safari
hii kukawa kimya. Hakuna kutembea wakiwa wamekumbatiana tena wala mabusu. Tunda
alijiweka pembeni kabisa, akishukuru Mungu jinsi yule dada alivyoongea vile
kuwa alishawataarifu kuna uwezekano wa kuchelewa nusu saa. Kwa hiyo watoe
nafasi ya hiyo nusu saa. Na wala Gino hakupitisha nusu saa.
Vilisikika
visu na uma tu hapo ndani na muhudumu akiongea kila wanapowabadilishia chakula.
Walikula mpaka ilipofika vyakula vya baharini, Tunda yeye akakataa asiwekewe,
nakubaki amekaa palepale. Safari hii hakutoka. Wengine walikula hicho chakula.
Wakaletewa na dessert tofauti tofauti wakiwa wamezipamba kiustadi ili kuvutia
familia hiyo ya Cote. Wakala.
“Unaonaje
Gino?” Akauliza bibi Cote baada ya kuomba muhudumu awapishe wabakie wao tu.
Gino akatulia kwa muda kama anafikiria. “Labda kwa kuwa mimi ni mpishi, naomba
niwe wa mwisho kutoa maoni yangu. Mrs Cote wewe umekionaje?” Akamrushia mpira
Tunda. Wote wakamgeukia Tunda. “Bado sidhani kama mimi ni mtu sahihi wakutoa
maamuzi ya chakula. Hapa nilipo nakaribia kutapika.” “Labla sababu ya samaki.”
“Nafikiri. Wewe Nana umeonaje?” Tunda akamrudishia mpira bibi Cote.
Akafikiria
kwa muda. “Sijui! Ni kama kuna kitu hakijakaa sawa! Lakini bado sijaweza kujua
ni nini!” “Excactly!” Akadakia Gino. “Kuna kitu kinapungua.” Akaongeza Gino.
“Ni nini Gino?” Akauliza Maya. “Ladha yake.” Akajibu Gino. “Labda tujue ni nini
ili tuombe chenye nafuu kirekebishwe, vingine vitolewe kabisa. Nimependa upangwaji
wa hawa.” Akaongea bibi Cote.
“Ila
sio juisi. Juisi sijapenda hata moja.” Akaongeza Tunda. “Hata dessert sio
nzuri.” Akaongeza Maya. “Kuku na samaki viko so so so...” Akashindwa jinsi
yakueleza, bibi Cote. “Plain?” Akadakia Net kama aliyeuliza hivi na hana na
yeye uhakika. “Yeah. Kuna viungo havijatimia. Vipo so plain! Yaani hakuna ladha
inayoeleweka!” Bibi Cote akakubaliana na Net. “Basi naomba mnipe tena nafasi
nyingine yakujaribu kutafuta watu wengine. Nimejifunza kutokana na kosa la leo.
Safari hii nitakuwa makini na muda. Nitahakikisha nakubaliana nao muda ambao
wote mtaweza kufika kwa wakati. Sio kama leo ambavyo nililazimishia ili Gino
awepo.” Tunda aliongea kwa upole na unyenyekevu kisha akaendelea.
“Naomba
mnisamehe kwa leo. Nilipanga kuwa flexible na muda sababu nilijua ni mimi tu na
Gino. Hata Maya sikuwa na uhakika kama angekuja. Alinipigia simu kwenye saa nne
asubuhi, akaniambia leo anakazi nyingi. Kwa hiyo sikujua kama hata yeye
angefika. Kwa hiyo sikuwa na wasiwasi kwa kuwa nilishawaomba wapishi wote
kuongeza muda zaidi. Yaani kutupa window ya kama nusu saa, nikiwaambia mtu
ambaye nataka anishauri, yaani Gino, angeweza kuchelewa. Wakasema ni sawa. Ndio
maana mimi sikuwa na wasiwasi tena. Kwa hiyo sio kosa la Gino. Tulikubaliana
hivyo.” Tunda aliongea taratibu akionekana kuishiwa nguvu kabisa. Alikuwa kama
mshitakiwa mbele ya hakimu.
“Mimi
sikujua kama mlikubaliana hivyo!” Net akajaribu kujirudi, lakini akawa
ameshachelewa. Alishamkera Tunda kuingilia kitu ambacho hata hakuuliza wakati
yeye mwenyewe alimwambia amemuachia apange! Tunda alijaribu kumuomba msamaha
mpaka na kumshika mkono ili tu atulie, lakini akaendelea kugomba! Alishamkera
Tunda, hakuwa na hamu tena. Tunda akanyamaza tu.
“It’s
okay Tunda. Nafikiri sisi tuliingilia, na tulitakiwa kuuliza kwanza.” Bibi Cote
na yeye akaongeza. “Basi wakati mwingine nitajitahidi kufanya au kumshirikisha
kwa karibu sana Maya ambaye anauelewa mzuri wa haya mambo ili awe ananishauri
kisha kuwajulisha kile ambacho tutakubaliana na wahusika wa kila idara kabla
hata ya siku yenyewe ya tukio. Kama ni kuonja au kuangalia tu. Ili mfahamu
kinachoendelea hata kama hamtaweza kuhudhuria.” Kimya.
“Kwa
mfano kesho, muda wa kuonja keki ni saa nane kamili mchana. Nimeshakubaliana
nao, na nitampa Maya, namba yao ya simu. Na yeye kuhakikisha huo muda, na Gino
aliniambia kesho atafika kwa wakati. Kwa hiyo kesho ni saa 8 mchana, ni uhakika
bila kuchelewa.” Akamalizia Tunda kwa upole kama aliyekubali kujivua majukumu
ambayo walimpa na kumthibitishia ameshindwa kuyafanya.
Hakuna
ambaye hakumuona jinsi alivyobadilika. Maya naye alishabadilika tokea sehemu ya
kwanza kaka yake alivyoanza kugomba. Wawili hao, Net na bibi yake wakajisuta
nafsini kwao kwa zamu. Pakawa pametulia kama kila mtu akiwaza lake.
“Mimi
naomba niwahi kurudi nyumbani. Sijisikii vizuri.” Akavunja ukimya Tunda. Tunda
anayetoka hapo siye waliyemuona muda mfupi aliyewapokea kwa shangwe huku
akiwaambia kwa wazi, amefurahi kuwaona. Alikuwa amejawa na furaha na nguvu.
Huyu Tunda anayewaaga sasa hivi alikuwa amechoka gafla na hakuna tena tabasamu.
Net akasimama ili
kumvutia kiti. Ile kusimama tu, akasikia kama chakula kinakaribia kutokea
mdomoni na puani. Akatoka pale kwa haraka na kukimbilia chooni. Akaanza
kutapika. Kwa mara ya kwanza tokea atue nchini hapo na mimba hiyo ambayo
imeshatimiza week 36, Tunda akaanza kutapika. Akatapika tena na tena mpaka akapiga
magoti hapo chooni. Akatapika mpaka akasikia nafuu.
Alipotoka
chooni akamkuta bibi Cote na Maya wamesimama nje ya choo alichokuwepo. “Are you
okay au tuite ambulance ikukimbize hospitalini?” Wakamuuliza wakionyesha
wasiwasi. “Hapana. Nitakuwa sawa tu. Nilikuwa nikitapika hivi hivi wakati
nilipokuwa Tanzania. Naona hii hali imenirudia. Nitakuwa sawa. Naona mimi
nirudi tu nyumbani. Nahitaji kupumzika.” Net naye akaingia kwenye choo hicho
cha kike.
“Vipi?”
Akauliza Net. “Nipo sawa. Naomba nirudi nyumbani nikapumzike.” “Nilifikiri yule
daktari alikupa dawa ya kuzuia kuta..” Kabla hajamaliza, Tunda akakimbilia tena
chooni na kuanza kutapika tena. Net akamfuata chooni na kumshika mbavu kwa
nguvu. Tunda akatapika tena na tena, mpaka akabakisha mate machungu. Akabaki
akihangaika kutoa hayo mate mpaka na machozi. Mlio wa mateso akiteseka wakati
akitapika, ulisikika na kutia wasiwasi wote waliokuwepo pale chooni.
Mwishoe
wakatoka chooni. “Pole.” Maya akamuhurumia. Wazi alionekana ameingiwa na
wasiwasi. “Asante. Lakini nipo sawa.” Tunda akasogea kwenye sinki kwenda
kusafisha mdomo na uso. “Unauhakika au twende hospitalini?” “Sidhani kama
kunatatizo. Nitakuwa sawa. Lakini nataka kurudi nyumbani.” Tunda akaweka
msisitizo. Wakatoka hapo kurudi nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net
alipofika tu karibu na mlango ili ashuke akamfungulie mlango, Tunda akajifungulia
mwenyewe mlango na kutoka kwa haraka na kuanza kutapika tena. Carter akatoka
kwa haraka akamsogelea Tunda pale alipokuwa ameinama akitapika. “Hey sweetheart?”
Carter akamgusa mgongoni kwa kujali. Tunda akatapika mpaka akamaliza. “Nipo
sawa.” Tunda akamjibu Carter huku akisimama maana alikuwa amepiga magoti. Net
naye akasogea. “Nikupe nini?” Akauliza Carter. “Nipo sawa babu Carter. Usiwe na
wasiwasi.” Tunda akampita Net, nakuingia ndani moja kwa moja chumbani kwao,
chooni na kufunga mlango kwa ndani.
Net
aliingia akikimbia mpaka chumbani kwao. Akamsikia akitapika chooni. Alipojaribu
kufungua mlango, ukawa umefungwa. Akajua ndio hatakiwi ndani maana huo mlango
haukuwahi kufungwa tangia Tunda anafika hapo. Akabaki akijaribu kusukuma kwa
nguvu kidogo. Tunda akamaliza na kukaa hapohapo chini pembeni ya choo.
Akamsikia akilia taratibu. Net akabaki amesimama nje. “Pole Tunda.” Hakujibu.
Baada kama ya dakika 5 hivi, akaanza tena kutapika.
Safari
hii hakukusikika kama anatoa tena kitu. Akahangaika hapo akitapika, mwishoe
kimya. Akamsikia amekaa chini tena. “Naweza kukusaidia.” Akaongea Net kwa
upole. Kimya kwa muda, akaona mlango unafunguliwa.
Tunda
akatoa nguo zake hapo, akaingia bafuni kuoga huku akilia taratibu. Hakutumia
muda mrefu bafuni, akatoka. Akavuta taulo lake, akaenda kujifungia ndani ya
chumba chake chakuvalia. Akabadili nguo humo ndani, akatulia kidogo. Ndipo
akatoka, moja kwa moja kitandani. Akajisogeza mwisho kabisa, kama asiyetaka
hata ajali ya kuguswa. Akajifunika vizuri mpaka kichwani, kimya. Mungu
akamsaidia, hapohapo akapitiwa na usingizi mzito kama aliyetoka kulima juani
kwa muda mrefu, akapata kivuli, akalala. Alilala Tunda, wala asijue alipo na
kinachoendelea ulimwenguni. Na kwa kuwa hakuwa na chakufanya mpaka saa nane
mchana siku inayofuata. Alishajipangia kulala tu.
Asubuhi ya Kwenda kuonja Keki.
Tunda alipofungua macho, akamuona Net amekaa
pembeni kabisa ya hicho chumba kwenye meza yake anayowekea kompyuta. Kwa kuwa
wakati mwingine huwa anafanya kazi zake hapohapo nyumbani mpaka usiku sana.
Kama hatafanya kazi zake hapo chumbani, basi kwenye ofisi yake ya hapohapo
nyumbani.
Tunda
alitulia kimya bila hata kujisogeza. Akamwangalia kwa muda kama anaye tafakari
kitu. Net alionekana amezama kwenye anachofanya. Tunda akageuza macho kwenye
saa ya ukutani. Ilishakuwa saa tano asubuhi. Akabaki kimya palepale kitandani
bila hata kujigeuza. Kwa utulivu ule, Net akajua bado amelala akatuliza na yeye
akili zake kwenye kitu anachofanya. Kwa asili Tunda alikuwa mtulivu sana. Kukaa
kimya, kusingemsumbua. Akatulia kimya kwa dakika nyingi tu.
Ghafla
Net akageuka kumtizama, macho yakagongana. “Nilijua bado umelala!” Akasimama
kumsogelea pale kitandani, alipokaribia kitanda tu, na yeye Tunda akatoka hapo
kitandani, akaelekea kilipo choo na sehemu ya kuogea. Net akamfuata nyuma. Tunda
aliingia chooni moja kwa moja akafunga tena mlango. Alikaa humo kwa muda
kidogo. Akatoka. Akamkuta Net anamsubiria nje ya choo.
“Umeamkaje?”
“Najisikia vizuri. Hali ya kichefuchefu imeisha.” Akajibu huku akielekea
kwenye sinki la kuoshea kinywa bila hata kumtizama usoni. “Gino amekutengenezea
uji na ndizi tayari. Unataka nikuletee huku?” “Hapana. Nitakwenda kula mezani
kama bado nitakuwa na muda. Lasivyo nitakuja kula nikirudi kutoka kwenye keki.”
“Naona kama labda mambo ya kuonja chakula uache tu!” “Kama ndivyo hivyo
mlivyoamua, ni sawa. Hamna shida.” Tunda akajibu kwa upole, lakini Net akahisi
anaharibu zaidi.
“Sio
kwamba ndivyo tulivyoamua. Wewe unaonaje?” “Kuhusu nini?” Tunda akauliza.
“Kuhusu kuonja hivyo vyakula. Kwa sababu..” “Net, mimi nipo sawa na kila
maamuzi mnayoamua. Nipo sawa. Na wazi sisi wote tunajua sipo kwenye nafasi ya
kuchagua au kufanya chochote kigeni kwenu. Naona uamuzi mlio amua wa mimi
kutoendelea ni mzuri.”
“Sio
kwa kutokukuamini Tunda! Ni kwa sababu ya hali hiyo ya kutapika. Hatukutaka
vyakula vingi tofauti tofauti vikutese kama jana! Lakini si vinginevyo.”
“Sawa.” Ikabidi tu Tunda ahitimishe. Maana alishapata jibu kuwa ni jambo
walilozungumza na bibi yake. Lakini ikawa kama imemuuma kwa namna nyingine. Akajua
hawakufurahia kilichotokea jana yake. Hakuzungumza tena. Akasafisha meno na
kuoga hapohapo bafuni ndipo akatoka kwenda kuvaa kwenye chumba chake. Safari
hii akamuona Net naye amenyamaza.
Alitoka
hapo kwenye chumba chake cha nguo na viatu kama mtu aliyevaa kutoka hapo ndani.
Alijifunika vizuri, akavaa sweta zito kidogo na viatu vyepesi kidogo kama buti
fupi za baridi lakini ndani vilikuwa kama vimetengenezwa maalumu kuleta joto.
Net akabaki akimtizama. “Natoka kwenda kutembea. Nitarudi baadaye.” “Naweza
kuja?” Akauliza Net kwa tahadhari. “Muda wa kwenda kuonja keki umekaribia. Na
mimi nataka nitembee bila kujiwekea kipingamizi cha muda. Sitaki kukuchelewesha
tena kama jana. Wewe endelea na ratiba zako tu. Mimi nahitaji kusafisha kifua
na kichwa.” Tunda akajibu hivyo nakutoka.
Alijua
Maya na bibi yake watakuwa kazini. Kwa muda ule hata Net alitakiwa awepo
kazini. Kuwepo pale inamaana yupo kwa ajili yake kitu ambacho Tunda hakutaka.
Hakutaka kabisa kuwa pale na Net. Bado ile hasira ya jana ilikuwepo na akamtibua
zaidi kwenye kumvua madara ya kuonja keki! Tunda akaona atoke hapo.
Ms Emily akamuona
akitoka chumbani. “Uji wako upo tayari.” “Nitakunywa nikirudi Emily, asante.”
Yule mama akabaki akimtizama. “Upo sawa Tunda?” Akamuuliza kwa upendo, Tunda akatingisha
kichwa kukubali. Akajiona machozi yanaanza kutoka, akajifuta na kutoka hapo
ndani akitembea kwa miguu tu.
Akiwa
hana kitu tumboni. Kutapika kote siku iliyopita bila hata kunywa maji, hasira
zikamfanya atembee parefu tu akiwaza hili na lile. Alijua lazima kuna mtu
anamfuata kumlinda. Hakujali wala kugeuka nyuma, akaenda kukaa sehemu ya peke
yake. Kwanza ilikuwa ni siku ya kazi, mida ile alijua watu wapo kazini, kwa
hiyo akapata utulivu wakutosha. Pia hakutoka na simu, akatulia. Alikaa hapo kwa
muda mrefu tu, zaidi ya masaa mawili. Baridi ikamtoa kwenye mawazo, akaona
arudi tu nyumbani.
Mazito Mengine Kwa Tunda.
T |
unda alianza kurudi nyumbani taratibu akijivuta. Hakujua kama alikwenda umbali mrefu vile! Sababu ya njaa akaanza kujisikia hata tumbo linamlemea. Akaanza kushindwa hata kunyanyua miguu. Akawa anaivuta taratibu. Akaangalia alipo na anapokwenda, akajua hatafika. Akasimama kabisa na kuanza kuangaza akitafuta mlinzi ambaye alijua yupo tu akimlinda. Akashangaa hata dakika tano hazijapita, dereva anakuja na gari. Akashukuru kuolewa na milionea. Japokuwa alimkera, lakini katika hilo akafurahia. Akajiambia atafia pazuri.
Bila maswali, likasimama pembeni yake, dereva akamfungulia mlango wa nyuma, akapanda. Hata yule dereva alijua wazi ni mlinzi pia. Akajiegemeza kitini, akavuta pumzi kwa nguvu akafunga macho huku akimpapasa mtoto wake. Tumbo lilikuwa ni kubwa haswa. Ghafla hali yakujiona amebeba mtoto mkubwa zaidi ikamjia, wakati alishakuwa akiambiwa na daktari, lakini hakuwa akiliona hilo. Siku hiyo ni kama ukweli ndio ulianza kumwingia na kulemewa ghafla.
Akafikishwa mpaka mlangoni, akamkuta Carter pale nje chini ya ngazi kama aliyekuwa akimsubiria. Akamfungulia mlango na kumshika mkono wakati anashuka. “Nimechoka!” Tunda akamlalamikia Carter. “Unaonekana mpaka usoni kama upo dhaifu. Twende ukale ndipo ukalale.” Akamshika mkono wakati anapanda ngazi.
Sura
ya Net siku Maya akimwambia atamtag Vic picha za Cote huko Facebook, ikamjia.
Akakumbuka kule kupaniki kwa Net baada ya Maya kumtaja jina lake mbele yake.
Akawa kama amekumbushwa kitu, akashtuka sana na kuingiwa hofu ya ajabu. “Siku aliyonikaribisha
hapa Net mpaka tukalala naye, wakati wewe upo jela na bibi yake akiwa safarini,
tulizungumza mengi sana. Moja ya tuliyozungumza ni Net alitaka turudiane. Wewe na
Chloe mlipita tu kwenye maisha yake, lakini moyo wa Net upo kwangu” Vic
akaendelea kwa ujasiri wote.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kumbe vile Tunda alipowafuata tu pale sebuleni, Carter alishamtumia ujumbe bibi Cote. ‘Vic amemfuata Tunda. Sijui ameingiaje getini, tumemshtukia yupo ndani akisisitiza ana kitu cha muhimu chakuzungumza na Mrs Cote. Wapo sebuleni wakizungumza. Nina hisia mbaya sana juu ya hili Ms Cote! Hali ya Tunda sio nzuri. Yupo dhaifu mno. Imebidi mlinzi wake aite usafiri kumrudisha nyumbani. Nimemshika mkono kumsaidia kupanda ngazi, sidhani kama yupo na nguvu ya kumkabili Vic kwa sasa.’ Carter akatuma huo ujumbe.
Bibi Cote, Maya na Net ndio walikuwa wamekaa wameletewa tu keki ndipo ujumbe ukaingia kwenye simu yake ya dharula. Hiyo simu alijua hakuna anayeitumia mpaka iwe dharula. Huwa haisubiri na wakati wote inakuwa na mlio. Akakunja uso na kuamua kusoma. Hata Net akashtuka baada yakusikia simu hiyo ikitoa mlio. Inamaana ipo dharula. “Is everything okay, Nana?” Net akauliza na Maya akanyanyua uso kumtizama. “Ujumbe kutoka kwa Carter!” Akajibu wakati anaanza kusoma.
“I
need my car ready, like yesterday!” Akasikika bibi Cote akiongea kwa sauti.
Huwa akiongea hivyo inamaana anatoka hapo na akifika nje, mlinzi awe
alishakimbia kwa dereva na kumwambia awashe gari, yaani akiwa anatoka nje, gari
imewashwa, na mlango uko wazi, yeye anaingia bila kupoteza hata sekunde moja,
gari liondolewe hapo.
Kwa Tunda.
H |
uku nyuma alipoanguka tu Tunda, kwa
kuwa aliangukia Tumbo rafiki wa Vic akashtuka sana na kuanza kupiga kelele.
Carter na Ms Emily wakakimbilia pale sebuleni walipokuwa wamekaa. Hapohapo Carter
akapiga 911 bila hata kumgusa Tunda aliyekuwa amelalia tumbo. Kufumba na
kufungua, nyumba ya Cote ikajaa magari ya wagonjwa zaidi ya matano. Police nao
pia wakajaa. Kwa kuwa Carter alisema ni hatari, Tunda ni mjamzito na ameangukia
tumbo akimshika haoni mapigo ya moyo.
Walitoka
hapo kwa mwendo kasi huku wakiwa wamewasha ving’ora kuashiria wapishwe na yeyote
barabarani na pikipiki za polisi nazo ziliandamana na hiyo gari ya wagonjwa kama
msafara. Wakiendelea kusafisha njia wakielekea hospitalini. Ikawa kelele ya
kuongeza wasiwasi.
“Ni nini kinaendelea!?” Net akauliza akionyesha wasiwasi mkubwa usoni huku akiomba Mungu asiwe Tunda. “Ron amenipigia simu sasa hivi na kuniambia nisizime gari wanarudi sasa hivi, tunaelekea hospitalini. Mrs Cote amekimbizwa hospitalini sasa hivi, hali sio nzuri. Wanajaribu kama wanaweza kuwahi kuokoa japo mtoto.” Akamuona Net anapepesuka kama anayetaka kuanguka. Akakaa chini kabisa. Ron ndio mlinzi wa bibi yake, inamaana zile ni taarifa za hakika.
Dunia ilisimama kwa muda. Akashindwa kufikiria kabisa, akakaa pale nje ya gari kwenye dirisha la dereva. Na dereva naye hakushuka. Akabaki akimchungulia na kumuuliza kama yupo sawa. Maana amri aliyoambiwa asizime gari, bibi Cote anarudi kukimbilia hospitalini. Asingethubutu kutoka hapo garini, asije kutokutwa ndani ya gari, nyuma ya usukani na kuharibu zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini kitaendelea? Usipitwe
na
muendelezo uliojaa mazito, mapya
na ya zamani yaliyokuwa yamewekwa sirini yatawekwa mwangani
v Vic amekiri hakudanganya. Anao ushahidi wa kulala
na Net baada ya kumuoa Tunda. Maya na Carter pia amewataja kama ni shahidi
zake. Na bibi Cote ndiye anayesimama kati ya penzi la Net & Vic! Kweli
mtoto ndiye anayemketisha Tunda na wakuu?
v Nani anaumiza kichwa cha Maya, binti mrembo
anayetamaniwa na kila mwanamme kwa urembo na pesa?
v Vic anaonekana kujua mengi na ya undani
juu ya Tunda, nani anamtumia safari hii?
Nani anayempa mbini makini za kumuangusha Tunda?
v Tanzania ilikuwa jela, safari hii nchini Canada
mahututi.
v Nini hatima ya Tunda na mtoto aliyembeba ambaye
ameanza kukosa hewa?
Yooote yatajibiwa. Usikose.
0 Comments:
Post a Comment