T |
![]() |
Akamuona
Sadiki bado amekaa vile vile kwenye kiti
chake, amefunga mkanda. Lakini kichwa
kipo kifuani kama kilichoshikiliwa na
ngozi tu iliyokuwa chingoni ikavutwa
mpaka karibu na tumbo. Tunda alishtuka sana na kuaanza kupiga kelele kwa hofu. Uzuri uso ulikuwa umegeukia kwengine, lakini aliona kichwa kikiwa kimening’inia na kushikiliwa na ngozi ndefu. Inamaana mifupa ya shingo ilikatika kabisa kwa ndani! Tunda aliendelea kupiga kelele huku akirusha miguu. “Wapo hai! Wapo hai!” Akasikia sauti kutoka nje, na mtu akirukia kwenye gari. “Nisaidieni
jamani. Niokoe!” Tunda aliendelea
kupiga kelele kwa hofu.
“Tulia usijitingishe. Gari imekaa vibaya. Unaweza kuniangusha na mimi au na wewe kujidhuru zaidi.” Ilikuwa
sauti kutoka nje. Tunda akajaribu
kutulia huku anaficha uso asimuone
Sadiki. Yule mtu akafungua mlango kwa
shida huku akijitahidi asije tumbukia mle ndani ya gari. Bado Tunda alikuwa ameshikiliwa na mkanda. “Jaribu kufungua mkanda kwa mkono mmoja, mkono mwingine nipe mimi ili usije kutoka kwenye kiti.” Yule mtu alikuwa amelala, huku anamchungulia Tunda ndani na kumpa hayo maelekezo.
“Mpo wa ngapi huko ndani?” “Wawili, lakini naona mwenzangu
shingo imekatika kabisa. Kichwa
kinaning’inia. Naomba nitoe tafadhali.” Tunda aliendelea kulia
kwa sauti ya juu na ya kupaniki. “Sasa usipaniki na wewe unaweza kuanguka, ukatua kwenye chuma kikakutoboa. Fuata maelekezo ukiwa umetulia tu, utatoka tu
salama.” Yule kijana alizungumza naye kwa kutulia. “Unahisi umebanywa popote?
Sitaki nikuvute, nikakuumiza.” Akasikika
mwenye uelewa ana anachofanya. “Hapana kaka yangu. Naomba nitoe tafadhali. Nivute tu.” Tunda aliongea kwa
hofu huku akiendelea kulia, asiamini
kama ule ndio mwisho wa Sadiki.
Alimvuta. Tunda akatoka akiwa ameshikilia pochi yake kubwa aliyokuwa ameipakata muda wote, yenye vitu vyake vyote. Lakini hakuwa na viatu. Alikuwa amevaa sendozi ambazo alizivua wakati anapiga mateke ndani ya hilo gari. Alipotolewa
tu pale, kama
aliyechanganyikiwa akaanza kukimbia
katikati ya watu walioanza kujaa pale.
Wakashangaa kidogo, akili zikarudi
kwenye gari ambako walijua yupo mtu
mwingine na pengine kuna vitu vya
thamani ndani. Wengine wakaanza
kuingia mtaroni lilipokuwepo limenasa
hilo gari ili kujaribu kuiba vitu ndani
ya hiyo gari ya Sadiki.
“Jamani tuweni
wastaarabu. Tuokoe maisha.” Mmoja
wao aliongea. “Mmeshasikia aliyebaki
huko amekufa. Kufa kufaana kaka.” Watu wakaanza kufungua
milango kujaribu kutafuta vitu vya ndani
na wengine walijaribu hata kung’oa
vioo na vifaa vingine vya hilo gari,
ilimradi tu kujinufaisha na hiyo
ajali. Hawakuishia hapo, wakaanza
kupekua maiti ya Sadiki mwenyewe
kuona kama anavitu mfukoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda alikimbia kama aliyechanganyikiwa. Alivuka barabara akipishana na magari asubuhi hiyo,
bila kujielewa. Alikimbia akilia, mwishoe akaenda kusimama mataa ya Shekilango akiwa anahema. Alisimama pale akiwaza huku akilia. “Sadiki!”
Hakuwa akiamini kama mwili wa Sadiki
aliouacha kwenye gari ndiye Sadiki yule
waliyekuwa wakiongea na kucheka muda
mfupi sana uliopita. Tunda hakupoteza
muda. Akavuka barabara kama anaelekea
Sinza, alitembea huku
akilia mpaka akakutana na taksii imepaki nje ya baa, alfajiri hiyo. Akamsogelea yule dereva, akamsalimia huku amejawa machozi, akaomba imrudishe kwenye ile hoteli
waliyokuwa wakiishi na Sadiki.
Njia nzima alikuwa akiendelea kulia. Alilia Tunda nakushindwa kujisaidia. Hofu ilimtawala, asiamini ni nini kinamtokea. Pale hotelini walikuwa wameacha baadhi ya vitu vyao. Sio vingi, lakini kwa kuwa yeye alijua jioni wangerudi, pengine wangelala au kila mmoja angekwenda kwake, hakubeba mzigo mkubwa zaidi ya hiyo pochi aliyokuwa ameshikilia hapo.
Dereva alimshtua kumwambia wamefika,
Aliponyanyua uso kuangalia nje ni kweli walikuwa wamesimama mbele ya
geti la ile hoteli. Akamlipa, na
kushuka taratibu kama anayeogopa
kitu. Alielekea moja kwa moja kwenye chumba chao bila kupita mapokezi.
Akafungua mlango nakuwasha taa kwa hofu. Akajikuta yupo peke yake. Akakusanya vitu vyote vya Sadiki visivyo na thamani. Akafunga kwenye mfuko na kwenda kuvitupa asubuhi hiyohiyo. Pesa zote na vitu vyake akatia ndani ya kibegi chake. Akaenda kulipia
hicho chumba mapokezi, akaondoka bila
kusema chochote, akarudi nyumbani
kwake.
Tunda alifika nyumbani kwake nakuanza kulia msiba wa yeye peke yake. Hana wakumwambia, hana wakulia naye. Inamaana starehe ndio mwisho! Sadiki alikuwa ni rafiki wa pekee kwa miaka hiyo miwili. Wawili hao waliishi kwa kuelewana katika starehe na ushirikina. Tunda hakuwa na kazi, ila kutapanya pesa ya Sadiki. Anakwenda wapi tena! Ataishije jijini hapo! Nyumba hiyo alikuwa amelipia kodi ya miezi mitatu kama walivyokuwa wamekubaliana na mwenye nyumba. Kodi ni ya miezi mitatu mitatu. Tena kwa dola. Ina kila kitu, tena vitu vya thamani tupu. Alijaza kuanzia mlango wa mbele mpaka nyuma.
Na Tunda
aliweka ulinzi wakueleweka kwenye
hicho kijumba ili kwamba akisafiri,
akute mali zake salama. Alikuwa
na kijana aliyekuwa akifika hapo kufanya
usafi kwenye hiyo nyumba. Kufua na
kupiga pasi. Chumba kimoja
alikigaramia, akakibadilisha na
kukifanya cha viatu, pochi na
nguo zake ambazo Tunda alimuelekeza
huyo kijana jinsi yakupangilia kwa ustadi. Tunda hakuwa akipoteza muda humo ndani endapo akitaka kuvaa kitu fulani. Nguo zilipangiliwa kwa rangi, aina, na za wakati gani. Ukiingia humo ndani ya hicho chumba tu, utafikiri duka la
wanawake kwenye nchi za walioendelea. Kulipangwa vizuri sana. Nyumba safi kila mahali na kila wakati.
Kulikuwa kumening’inizwa manukato yaliyokuwa yakijipuliza kila baada ya dakika kumi. Mishumaa hiyo hiyo ya
harufu ya Lavender ilikuwa imewekwa juu
ya meza hata chooni kwake. Spray za Lavender
pia alikuwa nazo kwa ajili ya kupuliza.
Ukifungua tu mlango kuingia ndani ya
hiyo nyumba, utakaribishwa na harufu kama sio ya pafyume ya Tunda, basi manukato
hayo ya Lavender
yaliyokuwa yameenea kila mahali.
Hakuwa akinunua vitu hovyo. Na usingekuta
takataka ndani ya nyumba ya Tunda.
Kila kitu kilionyesha pesa yakutosha. Na kwa hakika kila kitu
kingekuvutia macho kutazama, kasoro tu,
hakuna mtu aliyekuwa akiingia ndani ya
hiyo nyumba ila Tunda mwenyewe na huyo kijana wa usafi. Walinzi waliishia nje. Kila kitu mle ndani kilihitaji pesa ili kuendelea kuwepo kama kilivyo. Kuanzia yeye mwenyewe Tunda. Mwili wake, maisha yake ni pesa kubwa tu. Kijana anayetunza hiyo nyumba na vilivyomo humo ndani ya hiyo nyumba ya kupanga. Kuhakikisha hakuna vumbi wakati wowote vyote vilihitaji pesa. Vifaa na aina ya dawa anazoletewa Tunda kwa
ajili ya kung’arisha hivyo vitu, ni pesa.
Ulinzi wa hapo nje kuhakikisha yupo
salama wakati wote, nayo ni pesa. Na
pesa yote hiyo ilikuwa ikitoka kwa
Sadiki aliyemuacha kwenye gari akiwa
amekufa. Atafanyaje? Hakujua hata
kilichoendelea kule alipoacha mwili
wa Sadiki. Akaendelea kulia tu peke
yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Lakini hawezi kulia daima. Maisha lazima yaendelee. Kodi ilipwe, mfanyakazi amlipe na hiyo kampuni ya ulinzi pia ailipe ili aendelee kulindwa. Alikuwa na pesa ambazo alikuwa anapewa na Sadiki. Alikuwa na akiba yake. Lakini alichokuwa amejiapia Tunda, ni kutotangatanga mtaani
tena. Alipenda kwake,
akakusudia apatunze na daima awe na
kwake. Anafanyaje! Hilo ndilo likawa
swali lakumuumiza kichwa. Siku
zilizidi kwenda, akitumia akiba yake,
huku akifikiria chakufanya.
Swala la biashara ndio hakutaka kufikiria sana. Akajipa vipingamizi yeye mwenyewe. “Biashara hiyo naifanyia wapi? Napata wapi wateja na mimi sifahamiki na yeyote yule!? Kwanza kuongea sana sipendi. Kichwa kinaniuma.” Akajiambia Tunda akiwa peke yake na kuzidi
kujikatisha tamaa. Akaamua kutupilia
mbali maswala ya biashara.
Akaanza kufikiria kumtafuta Sadiki mwingine.
“Nitapata wapi mwanaume anayejua kuhonga kama Sadiki?” Tunda akajiuliza nakuzidi kuombolea. Sadiki alikuwa akitoa pesa bila maswali. Akimuomba pesa hana maelezo mengi kwake, yeye anatoa tu. Akalia bila kufikia mwafaka juu ya hatima
yake. Mwishoe akajua anapoteza tu
muda. Lazima maisha yaendelee. “Kwani Sadiki nilimpataje? Safari moja, itaanzisha nyingine.” Akajiambia Tunda na
kujipa moyo. Akafurahia na kujipongeza
kuwa na kwake.
Hakuna mtu
anayemfahamu kama alikuwa na Sadiki,
hasa ndugu za Sadiki. “Wangenipora kila kitu
humu ndani, au hata kunifukuza. Heri
napata pakufikiria nikiwa
kitandani kwangu.” Tunda
akajipongeza kwa hilo. Waliomfahamu yeye
na Sadiki, walijua anaitwa Ani, basi.
Hawakujua anakotokea, au anakoishi. Kwanza hawakuwa wakionekana pamoja
hadharani. Na endapo
ilipowalazimu kuwa pamoja, kama
wanakwenda kwenye baa zake, kama
hakubaki ndani ya gari, basi alishuka
naye, nakutafuta sehemu ya kukaa,
wakati Sadiki akifanya shuguli zake
kwenye hizo baa zake. Tunda kimya.
Hataongea chochote, na yeyote. Hata
muhudumu akimsogelea, hatamsemesha
kitu.
Alijua
wafanyakazi wote wanamfahamu mkewe
Sadiki kwa hiyo hakutaka kujichanganya, ili kuepuka historia yake kujiridua
kama alivyotendwa na mama yake alipomuadhibu kwa ajili ya baba Tom. Alijiapia
na kujiwekea huo usemi, “Ukitaka kula
na kipofu, usimshike mkono.” Hakuiba
kwa kelele wala fujo. Maadamu
alikuwa akipewa mapesa, akawa
akimsukumia Sadiki kwa mkewe pia, ili
asije akapokonywa akiwa anamuhitaji. Hiyo
tabia hata Sadiki aliipenda sana. Aliona
Tunda anaheshimu ndoa yake. Hapakuwa na
ugomvi.
Sehemu
walizokuwa huru kuongozana naye ni kwenye club, tena usiku. Watatafuta sehemu
yao watakaa. Au wakiwa wanakwenda mziki.
Basi hapo utawaona pamoja. Au
wakiamua kutoka nje ya jiji. Wakijua
hakuna anayewafahamu, basi hapo
utawakuta hata wakitembea wameshikana
mikono na kucheka kama wapenzi wa
kweli. Lakini si vinginevyo. Katika
hilo Tunda hakuwahi kujisahau.
Historia yake ya nyuma ilimfanya
asijisahau. Akakumbuka alivyoishia
hospitalini akiwa hana mtu na wala hana
pakwenda.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
akavuta pumzi kwa nguvu nakujipongeza.
Akajiona ameibuka mshindi. Akakaa
kutoka pale alipokuwa amejilaza. Akaangalia chumba chake chote. Akafurahi kujiona yeye ndio mmiliki na hatakaa akafukuzwa pale, labda ashindwe kulipa kodi. Akavuta pumzi kwa nguvu. “Ani amekufa na Sadiki.” Akajiambia kwa huzuni na kuanza kulia tena.
Atafutaye
Hachoki.
Kulikuwa na club moja ipo kati ya Osterbay na Masaki. Alikuwa akipenda kwenda na Sadiki. Japo hawakuwa wakinywa pombe, lakini walipenda kuwepo huko mara kwa mara sababu ya bendi iliyokuwa ikitumbuiza hapo nyimbo nzuri za zilipendwa, Sadiki alipenda sana kwenda hapo kwa ajili ya hiyo bendi. Walipenda mandhari yake pia. Kuliuzwa vinywaji na chakula kwa bei ya juu kwa hiyo walijiona wapo salama. Hawakutegemea kukutana na wasio na shuguli huko. Wakati wote wanapokuwepo
hapo, walijiona wapo salama.
Walikuwa
wamejiwekea sehemu yao. Kwenye
kona kabisa, gizani kidogo. Wakifika
hapo, watakaa wakicheka kwa muda
mrefu tu. Watakula huku wakisikiliza
zilipendwa. Basi hapo Tunda ndipo
alipokuwa akimsikia Sadiki akiimba
kwa furaha yote. Tunda alishakutana na wenye pesa zao huko. Akajua huko
huko ndiko kwakuanzia kupata wanaume.
Kwa kuwa alikuwa akijua vitu vya
thamani, kwa kumuangalia tu mtu, alijua huyu
anayo pesa au la. Kuanzia saa
aliyovaa mkononi, kiatu au hata tu
shati alilovaa, Tunda aliweza kujua
kama mwanaume atamfaa au la.
Miezi
miwili ilikuwa imeshapita tokea kutokea kwa ajali mbaya
iliyosababisha kifo cha Sadiki, Tunda
akiwa amejifungia tu ndani akiwaza
maisha yake. Ni nini chakufanya ili
kuendelea kujiingizia kipato chakumfanya
aishi mjini vizuri, tena pale pale
kwake. Alikuwa akiendelea kuishi kwa
akiba ya pesa iliyokuwa imesalia kipindi
cha uhai wa Sadiki. Akajua asipokuwa mwangalifu, ataishiwa kabisa na kufukuzwa pale anapoishi. Lazima kuchangamka. Ndipo akili ilipomjia kwenda kwenye ile Club kuomba kazi ili apate mwanaume mwingine kama Sadiki atakayemuweka mjini.
Kwa mara ya kwanza tokea msiba wa Sadiki, akatoka kwenda Salon. Akabadilisha hata aina ya nywele. Akaweka kucha nyingine nzuri kama zake.
Akarudi nyumbani sasa
kujitengeneza vizuri huku akivuta
muda akitegea kufika pale mida
ambayo alijua hata
mmiliki angemkuta. Hakika
alipendeza. Alivaa vizuri,
akajitengeneza kutokana na rangi yake ya
mwili. Aliporidhika na muonekano wake
yeye mwenyewe na muda ule, ndipo akatoka
sasa kuelekea kwenye hiyo club.
Dereva wa Uber
aliyefika hapo kumchukua, ilimshusha
hapo club ikiwa imeshafika saa tatu
usiku. Alikuta watu wengi tu. Ilikuwa
siku ya ijumaa. Watu wameshatoka
makazini, wanasheherekea weekend.
Alitembea taratibu kupita
watu waliokuwa wamekaa nje
wakisikiliza bendi iliyokuwa ikitumbuiza
taratibu tu, akaingia mpaka ndani
mapokezi. Alimkuta mrembo aliyempokea
kama aliyemdharau Tunda.
Alipomuulizia mmiliki, akamjibu
bila hata kumtizama. “Yupo ofisini kwake.” Tunda akatulia kidogo, kisha akaomba kwenda kumuona. Yule dada akawa kama
amepatwa wivu alipomtizama tena vizuri
na kugundua Tunda amekamilika kimuonekano,
jeuri ikaongezeka. Akamkatalia kwa kumwambia bosi yupo busy,
labda afike hapo siku za jumatatu
asubuhi, weekend anakuwa busy sana.
Hapokei wageni.
Tunda hakubisha. Akaomba namba zake za simu, pia akamkatalia. Tunda hakuongeza neno, akatoka pale na kwenda
kutafuta meza upande mwingine kabisa,
sio ule aliozoea kukaa na marehemu
Sadiki. Baada ya muda mfupi tu,
muhudumu akamsogelea kumuuliza
anataka kinywaji gani. Tunda
akatabasamu. Akaagiza maji na kutumia
akili ya haraka sana. “Na wewe upate
kinywaji chochote, halafu mwambie
Kinny, anamgeni wake hapa.” Tunda
aliongea taratibu. Kinyami
“Unamaanisha Kinyami,
bosi mwenyewe?” Yule muhudumu akauliza kwa kubabaika kidogo kwani hilo lilikuwa jina la kwanza la mmiliki, na aliitwa hivyo na marafiki zake wa karibu sana. Vijana wenzake waliokuwa wakifahamiana tokea zamani. Hata wao wafanyakazi wenyewe
hawakuwa wakimwita hivyo.
“Ndiyo. Nenda kamwambia Fina anakusubiri. Na
akichelewa, nitaondoka, sitamsubiri na
siwezi kurudi tena.” Tunda akaweka
msisitizo. Kwa haraka sana yule muhudumu
akaondoka pale. Baada ya muda mfupi,
yule muhudumu na mmiliki ambaye ni Kinny mwenyewe, wakafika pale kwenye meza ya Tunda. Kinny akababaika kidogo mbele ya Tunda aliyekuwa akimtizama kwa kujiiba huku macho yapo kwa muhudumu aliyekuwa akiweka maji hayo kwa kubabaika mbele ya bosi wake. Alifuta ile chupa ya maji mara kadhaa. Kisha akaweka glasi mbele, pembeni, kushoto, ilimradi akawa ameshasahau wapi aweke hiyo glasi kwa kuwa bosi wake alikuwa akimtizama.
“Acha tu,
mimi nitamimina hayo maji kwenye glasi.” Kinyami au Kinny kama
rafiki zake wa karibu walivyozoea kumuita, akatoa hiyo amri kwa muhudumu wake. Akaelewa anatakiwa kupisha hapo
kwa haraka. “Karibu.” Akamkaribisha Tunda, Tunda alitoa tu tabasamu, akarudisha macho kwa Kinny, muhudumu akaondoka.
“Habari Fina? Sijui ni sawa au amekosea kuniambia?” Akimaanisha muhudumu wake
aliyekwenda kumwita. “Umepatia.” Tunda
akasimama na kumpa mkono na yeye.
“Karibu sana.” Bado alikuwa ameshika mkono wa Tunda akiuminya. Laini kama sponji! Tunda akacheka taratibu huku akimtizama na yale macho yake. Kinny akajishtukia, akaachia mkono wa Tunda kwa haraka. “Karibu ukae.” Tunda akarudi kukakaa na yeye akakaa “Mbona umeagiza maji tu
wakati weekend ndiyo inaanza?”
Tunda akacheka kidogo na kujibu taratibu.
“Maji
yanatosha.” “Karibu sana.” Kwa vile
alivyomuona Kinny amebabaika mbele yake,
Tunda akabadili mawazo yakuomba kazi
pale kwenye ile club. Utizamaji ule na kushindwa
kuachia mkono wake kwa haraka, akajua
ameshavutiwa naye na ameshamthaminisha.
Akaona kuomba
kazi, nikuanzia chini sana. Uthamani
wa Tunda ukapanda kwa haraka,
ujasiri ndani yake ukapanda. Akanywa maji kidogo.
Vile tu alivyoishika ile glasi, kucha yake kidoleni, cheni iliyoning’inia hapo mkononi, hata Kinny alijua anaongea na mdada wa hali ya juu. “Najua hatuna miahadi yeyote ile, lakini nilitaka tuzungumze biashara.” Tunda akaanza
taratibu huku akili yake ikiendelea kuchemka
kwa haraka akifikiria nini chakumwambia Kinny aliyekuwa akimsikiliza kwa
makini. “Sitakuibia muda wako
mwingi.” Tunda akaendelea taratibu. “Hamna neno. Hata hivyo sina kitu chakunifunga na
kunifanya nisiwepo hapa na wewe. Una
habari gani njema?” Tunda akatoa
tabasamu huku akifikiria akatazama upande
waliokuwa wakitumbuiza. Walipokuwa wamesimama waimbaji. Kinny naye akageuka.
Kulikuwa na
baadhi ya watu ambao walionekana
pombe zilishaingia kichwani,
walisogea kucheza karibu na ile bendi. Mmoja alifanya vituko, Tunda na Kinny wakajikuta wakicheka kwa pamoja. Kinny asijue cheko ile ya Tunda ni yakuzuga tu. Yupo kwenye kufikiria
kwa kina, nini chakumwambia
na kilete maana. Akakumbuka kwenye baa
ya Sadiki, ni nini alikuwa akinunua chamuhimu
na nini hata hapo kinatumika sana.
Akanywa maji na kumtizama Kinny. “Unanunua
wapi bia zako?” Akamuuliza taratibu tu. Kinny
akawa kama anafikiria. “Mmmh! Huwa wananiletea hapahapa kutoka kiwandani. Vipi? Una dili nzuri nini?” “Wanakuuzia
kwa bei gani?” Tunda akauliza tena.
Alipomtajia, Tunda akakunja uso. “Vipi?” “Mimi naweza kukupatia kwa bei ya chini zaidi, na ukitaka, wanaweza kukuletea pia.” Kinny akacheka huku akimtizama. “Wapi huko
kwenye neema, Fina?” “Wewe sema kama
utataka.” “Ila isiwe magendo
tu. Sitaki matatizo baadaye.” Kinny akatahadharisha. “Hakuna
magendo. Watu haohao wanaokuletea wewe
hapa kama wafanyakazi wa kicho kiwanda,
ndio haohao watakao kuletea ila kwa bei
poa. Wanatoa hapohapo kiwandani, tena
kwa halali. Ila wao kama wafanyakazi
huwa wanauziwa kwa bei ya chini sana, na
kwa kuwa huwa wakati mwingine ni kama
wanapewa bure, basi wanakuwa na mzigo kwenye
maduka yao, wanauza kwa bei nzuri.
Kwa risiti kabisa. Wala sio wizi.”
Tunda akaongea kwa uhakika kabisa
kumuaminisha. Kinny akatabasamu.
“Na wewe unapata kiasi gani kwenye hiyo?” Tunda akacheka kidogo. “Wewe
usijali. Tunajuana na wao.” “Kwa hiyo
tukimalizana hapa na wewe, tukaachana
leo, ndio sitakuona tena?” Akauliza Kinny na
tabasamu la uchu usoni. Tunda akajua
tayari, akaona amzungushe kidogo. “Usiwe na wasiwasi. Sio wababaishaji hata kidogo. Wakishajua ratiba yenu ni lini mtahitaji mzigo, hata wewe huna haja ya kuonana nao. Inakuwa wao na mtu wako wa stoo tu.” Akajidai akili ipo kazini.
“Mbona umeanza na
habari njema, halafu unamaliza na
habari mbaya?” “Kwa nini tena? Mimi nilijua utafurahia punguzo la bei!” Tunda akauliza huku akicheka. “Huko kutokuonana, ndio habari mbaya.” Tunda akacheka sana. “Mimi nilijua wewe upo busy, hupendi usumbufu. Unaonana na watu muhimu tu.” “Wewe umeshakuwa mtu muhimu kwangu, Fina. Ningependa tuje kuonana tena.
Huwezi jua ni nini kitazaliwa baada ya
hapa.” Tunda akacheka na
kuinama kama anayefikiria.
“Eti Fina?” “Basi leo ni mimi ndio nimekutafuta kwa shida yangu. Na wewe nakupa ruksa kunitafuta kwa wakati wako.” Kinny akacheka
kwa kuridhia. “Maswala ya biashara mimi na wewe tumeshamalizana. Agiza chakula
hapa, kula wakati unanisubiria
nitakuitia mtu anayehusika na manunuzi
ya vinywaji. Panga naye kila kitu.
Muelewane. Nisubirie mimi nivute muda
kidogo, wakati nasalimiana na wateja
wangu. Halafu nitakuja
kukuangalia tutapanga kutokea
hapo. Au una haraka?” “Hapana. Nitakusubiri Kinny.”
Hiyo sauti ikamfanya Kinny alambe midogo. Tunda akacheka sana. “Kinny wewe ni mtundu sana.” “Kwa nini tena?” Na yeye akacheka huku anasimama. “Nitarudi
kukuangalia. Usije nikimbia tu.” “Utanikuta hapahapa.
Usisahau kuniitia mtu wa manunuzi.” “Ona sasa! Sauti hiyo imenifanya mpaka nimesahau.
Acha basi Fina!
Unanishika miguu!” Tunda alizidi
kucheka, Kinny akaondoka huku na
yeye akicheka.
Alionekana ni mcheshi. Alikuwa akipita kwenye meza baadhi akisalimia. Tunda alimuona jinsi anavyocheka kwa sauti huku akigonga mikono na baadhi ya wateja. Tunda alikuwa kazini na mahesabu makali.
Akaendelea kumtizama kila
anayezungumza naye. Kuanzia
mkononi mpaka miguuni. Taratibu.
Akagundua anasalimiana na watu
ambao na yeye anania nao. “Huyu
mbaguzi huyu! Mbona anasalimiana na
wenye pesa tu?” Tunda aliwaza huku
akimsindikiza kwa macho. Baada ya
muda akamuona anaingia ndani.
Tunda akaendelea kuwaza akiwa peke yake pale mezani. Akapanga hili na kufikiria lile. Akamsogelea kijana aliyejitambulisha kuwa anahusika na vinywaji. Tunda akamwambia
akae wazungumze. Akaanza kumuuliza maswali kwa makini. “Huwa mnachukua bia mara ngapi kwa juma
na kwa kiasi gani?” Yule kijana
aliendelea kujibu kwa makini. Tunda
hakuonekana mshamba au hajielewi.
Alijibeba kimaana. Unaweza kufikiria ni
msomi mwenye mipango mizito sana.
Aliendelea kumuuliza yule kijana
maswali yaliyomfanya afikirie kidogo,
huku akimtizama na kumsikiliza
kisha anaandika kwenye
simu yake. Mwishowe akachukua namba yake ya simu na kumwambia kesho atampigia. Yule
kijana akashukuru, na kuondoka.
Baada ya kama dakika 45, Kinny akarudi. “Umechoka?” “Kelele nyingi sana hapa kwako. Huwa sipendi sana kelele, hasa zikiwa za muda mrefu na mimi nikiwa kama hivi peke yangu. Nahisi ni kama wapo wote masikioni kwangu. Naomba nikuage, tutakutana wakati mwingine.” Akajilalamisha
kwa deko. “Basi
acha nikusindikize kwenye gari yako.” “Natumia
taksii tu.” “Basi naomba
bahati ya kukusogeza
mpaka nyumbani.” Tunda
akacheka. “Nisogeze mpaka Mlimani
City tu.” “Mzee mkali nini?” Tunda akacheka huku akisimama, hakujibu hilo. Wakatoka pale.
Tunda aliwaza jinsi yakumuanza Kinny kama alivyomuanza Sadiki kwenye gari. Kinny alionekana sio limbukeni. Mtoto wa mjini, anayejua wanawake. Hakutofautiana sana na Sadiki aliyembadilisha zaidi, hasa kimavazi,
lakini Kinny yeye
alionekana bado kijana mdogo kidogo
halafu mjanja. Wakapanda kwenye
gari ya Kinny, akaondoa gari.
Wakajitahidi kuzungumza mambo ya
kawaida wakiwa njiani. Tunda alikuwa
amekaa pale huku
akimpigia mahesabu.
Alikuwa makini sana na kila anachojibu au kuchangia ili asiropoke na kujichanganya baadaye. Akawa mchache wa
maneno, msikilizaji mkubwa. “Unaonekana
wewe ni mtulivu sana Fina?” “Kelele
nyingi huwa zinanichosha akili.” Tunda akajibu taratibu na tabasamu usoni. Kinny akamtizama na kutoa tabasamu lililoficha maneno. Tunda akacheka. “Wewe ni
mtundu Kinny.” “Jamani! Siruhusiwi
kutamani? Labda uniambie ni mali ya mtu.” Tunda akacheka cheko zuri bila kuongeza neno. Akageukia dirishani.
“Finaaa! Hutaki kelele mwenyewe! Basi niambie
nitakuona wapi?” “Si tuko wote hapa?”
“Hapa sio
patulivu Fina! Nataka na mimi nipate
huo utulivu.” Tunda akacheka sana. “Hata hapa ni patulivu, ni
wewe tu.” “Kwamba nina kelele?” “Hapana. Simaanishi hivyo. Namaanisha ni wewe ndio unapadharau. Lakini pana utulivu wakutosha kabisa. Ushindwe tu wewe
mwenyewe.” “Wewe unaweza kupata utulivu
humu?” “Kabisa.”
Kinny akamgeukia. “Nini sasa? Mbona kama
huniamini?” “Nahisi kama unanisukumia barabarani, kuninyima kukuona tena, au kutoonana hiyo sehemu tulivu. Naona unanibania Fina.” Kinny akajilalamisha.
“Tatizo lako umekariri Kinny.” “Kweli?” “Kweli tena.”
Tunda akamuhakikishia.
Kinny asiamini na kuendelea kuuliza akicheka tu. “Lakini wewe unahisi hata hapa
ni patulivu?” “Sana tu.” Tunda akazidi
kumuaminisha. Kinny akamtizama. Wote wakacheka. “Nakupa ruksa kunisahihisha.” “Usije ukalia tu.” Kinny akacheka sana mpaka akagonga usukani.
“Unavyojiamini
Fina!” “Mimi
nimetoa angalizo tu. Mida hii ni ya kazi kwako! Usije ukanililia, wakati
unatakiwa kazini.” “Mimi mtoto wa kiume
Fina, silii kishamba.” Tunda akamtizama,
akageuka dirishani huku akicheka. “Mbona unanicheka?”
“Nimefurahi tu.” “Furaha hiyo ni ya
kunicheka mimi tu. Sasa hapa lazima
tumtafute muongo nani. Naegesha gari
mwisho kabisa. Tubaki mimi na wewe.”
Tunda akamtizama tena.
“Au umeingiwa na
hofu?” Kinny akauliza
kama aliyemkamata Tunda. “Utashindwa wewe! Nakuhurumia.” “Nimechezwa mwenzio, tena na kina mama wa kizanzibari,
kisha wakanikabidhi mke.” Kinny akajisifia, nakumfanya Tunda acheke zaidi. Alicheka Tunda
hakutegemea maneno ya Kinny. Kama utani,
Kinny akaegesha gari mwisho kabisa
alipoona hakuna magari mengine pembeni
yao. Akatulia na kumgeukia Tunda.
Akamuona Tunda anapitisha mkono pembeni yake, akalaza kiti chake taratibu huku akimtizama kwa macho yake. “Oooohooo!” Kinny akatania kwa kutoa huo mlio kwamba ameingia hatarini. Baada ya dakika 2, maneno yalimwisha
akabaki akigugumia, Tunda akiwa amepiga magoti kwenye kiti chake. Akamwachia akabaki akimtizama
vile alivyokuwa akiweweseka pale kitini. “Nilaze kabisa?” Kinny akauliza huku anababaika, asijue ashike wapi. “Au tuhamie nyuma?” Tunda akaanza kucheka. Akachukua pochi yake. “Acha hizo
Fina bwana!” “Nilikuonya usining’ang’anie Kinny. Huu ni
muda wangu wakwenda kulala, na wewe rudi kazini.” “Daah!” Akavuta kiti akakaa huku
akijifunga zipu ya suruali vizuri.
“Tafadhali usiondoke Fina.” “Hapana Kinny. Rudi
kazini.” “Sio vizuri Fina! Usiniache hivi nusunusu.” Kinny akawa kama ameshachanganyikiwa. “Nimekupa ruhusa yakunitafuta. Nipigie simu, tupange vizuri. Wewe mtu na heshima zako, kwa nini unataka mambo ya kwenye gari
bwana? Nipigie.” Tunda
akachukua kalamu kutoka kwenye
pochi yake. Akamvuta mkono,
akaandika namba yake ya simu bila
jina kwenye kiganja cha Kinny, kisha
akafungua mlango nakutoka hapo
ndani ya gari bila kuaga.
Tunda tena mtaani. Safari hii ni
Fina, akitafuta pesa ili kuweza kuishi mjini.
-
Je, Kinny ataweza kuvaa viatu vya Sadiki?
-
Mwisho wao ni upi?
-
Nini kitaendelea kwa Tunda aliyekusudia kufa na kupona ili aweze
kuishi mjini, tena kwa kujinafasi?
Endelea kuwa na Tunda katika sehemu ya 12.
Safiii
ReplyDelete