W |
![]() |
“Sijawahi kula ugali na nyama ya kuku vitamu hivi!” Sadiki akacheka wakati Tunda akiendelea kula kama anayelishwa. Alikula mpaka akamaliza. “Sasa nasikia usingizi.” “Wewe jipumzishe hapohapo kwenye
mkeka. Ngoja nikamtafute Babu.”
Hakujua kilichoendelea mpaka
alipoamshwa ilikuwa usiku. Giza.
Sadiki akamwambia waondoke kurudi
Dar. “Mbona miguu inamichanga kama wa baharini au ziwani!?” Tunda aliamka akiwa hana viatu, michanga miguuni na mapajani kama ameloa
kidogo. “Twende, tutazungumza
kwenye gari.” Tunda akasimama.
Alikuwa palepale alipokuwa amelala
baada ya chakula. Kwenye mkeka kama sebuleni. Akaangalia kulia na kushoto, akajikuta yupo yeye na Sadiki tu.
“Twende Ani.”
“Hatuagi!?” Tunda akauliza. “Babu
yupo na wazee wenzake sasa hivi,
wanafanya ibada. Tutarudi wakati
mwingine.” Akamsaidia kusimama. Alipoingia tu kwenye gari, akalala tena usingizi kama wa mtu aliyefanya kazi nzito sana. Hakushtuka mpaka tena Sadiki alipomwambia wamefika hotelini. “Tumefika
Dar!?” Tunda hakuamini. “Umelala
sana. Twende ukapumzike
ndani.” Tunda akashuka. “Acha nioge kwanza kabla sijalala.” “Kabla hujaoga, njoo kwanza hapa kitandani.” Tunda akashangaa anamtaka kimapenzi hata kabla hawajaoga!
“Wachafu hivi!” “Hivyo hivyo nakutaka
Ani. Njoo kimapenzi changu.” Tunda akacheka, akavua nguo kwa haraka na kumkimbilia Sadiki.
Akajiona anauchu naye kama hawakuwepo hapo kitandani usiku uliopita. “Nina hamu na wewe!” Tunda akajikuta akilalamika. “Naomba na leo tulale wote.” Tunda akaendelea kubembeleza. “Sawa. Lakini haya maisha ya hotelini ni yakubadilisha kabisa. Tukinunua tu kitanda, tunahamia kwetu. Mimi na wewe.” Hapo Tunda hakujibu, akaendelea kumng’ang’ania tu. “Tukitoka Arabuni ndio tunahamia kwetu. Si ndio mama?” Sadiki akaweka msisitizo. Tunda akacheka tu. Akawa kama amepagawa hapo kitandani. Nguvu mpya na shauku kwa Sadiki ikaongezeka. Akatumia ujuzi mwingi hapo akitaka Sadiki afurahi. Alipochoka Sadiki ndipo akamwambia wakaoge, ndio walale. Bila kubisha, akaongoza bafuni kuoga, na kurudi kulala.
Tunda Mpya.
T |
unda
akabadilika kabisa. Akawa mtiifu sana
kwa Sadiki. Usingemkuta akibisha
chochote anachoambiwa na Sadiki. Mapenzi
yakaongezeka wawili hao, hamu ya kuwa
pamoja ikaongezeka. Tunda
akawa mwanamke wa hapo
hotelini. Akitoka ni kujinunulia vitu
vyake, saluni, na kurudi hapo akimsubiria Sadiki.
Alimpenda na kumnyenyekea huyo Sadiki, utafikiri Mungu wake. Hakuna kitu angeambiwa na Sadiki, akabisha. Mpole na mnyenyekevu. Kwanza
usingewakuta wanabishana.
Wakashugulikia hati
zao zakusafiria na Visa,
Tunda akajifunika kama mtoto aliyepitia madrasa, wakaingia Arabuni. Ni kweli Sadiki alikuwa na pesa. Walifikia kwenye hoteli nzuri sana. Walijifungia hapo kama siku tatu. Wao tu. Hakumuona Sadiki akipiga hata simu kwa mkewe. “Umemwambia mama Amini kuwa tumefika salama?” “Mimi nilijua unataka muda na mimi! Sasa unamleta huku mama Amini wa nini!?” “Kweli mpenzi wangu.” Tunda akatulia na kuendelea kufaidi yeye.
“Tukirudi
lazima tukatoe sadaka.” “Sawa.” Tunda akakubali
huku akimchezea taratibu kifuani. “Na vitanda vikifika tu nchini, tunahamia kwetu.” Tunda akacheka, kisha kimya. “Au hutaki kuishi na mimi?” “Nataka Sadiki.” “Lakini isiwe hotelini.” Akasisitiza. Tunda akaendelea kumchezea taratibu. Walizunguka wakitafuta thamani ya dhani za Tunda bila kuchoka. Na Sadiki
naye alikuwa akinunua kila kitu alichotaka Tunda bila kupinga. Kwa mamilioni ya pesa
ya kitanzania aliyokuwa amebadili kwa dola. Tunda akapata kila alichokuwa akitamani.
“Umefurahi sasa?” “Sana.” “Mimi nataka ufurahi.” Wakatafuta njia nzuri ya kuvifikisha
hivyo vitu mpaka nchini Tanzania.
Napo hapo pesa yakutosha ikamtoka Sadiki. Walipohakikisha vitu
vyao vimepakiwa melini, ndipo
wakarudi nchini Tanzania. Hotelini
tena. Sadiki alikaa hapo hotelini
siku moja, siku inayofuata akamuaga
Tunda. “Nitarudi kesho jioni.
Ujiandae tutakwenda kutoa sadaka
ndipo turudi kwa babu Chonde.” “Sawa.”
Bila kuuliza ni wapi wanakwenda kutoa
hiyo sadaka, Tunda akakubali.
Taka Cha Mvunguni,
Sharti Ainame.
Waliendesha mpaka makaburi ya Sinza. Akaegesha gari yake mbali kidogo
na makaburini. “Tushuke hapa.” Sadiki akiwa ameshika mfuko mkubwa kidogo wenye baadhi ya
vitu aliokuwa ameacha hapohapo kwenye gari wakati anaingia kwa Tunda, akamfungulia
Tunda akashuka garini, wakaanza
kutembea wakielekea yalipo makaburi,
Sadiki akiwa na ule mfuko. “Tunaenda wapi Sadiki?” “Hapo ndani makaburini.” Tunda akashtuka kidogo. “Usiku huu makaburini! Mimi naogopa.” “Usiogope. Tupo wote. Na wala hatutakaa muda mrefu. Sawa?” “Nishike mkono basi.” Sadiki akacheka akamshika mkono vizuri huku
akimtuliza kumtoa hofu. Akaangalia kushoto na
kulia kama asiyetaka mtu awaone,
wakaingia ndani eneo la makaburini.
Wakaelekea mwisho kabisa kwenye makaburi hayo, Sadiki akamwambia hapo panatosha. “Ndio tunafanya nini huku!?” “Wewe fuatisha kila kitu ninachofanya. Ni rahisi tu.” “Kwani ulishawahi kufanya hivi?” “Ani kwa maswali!” “Nataka kujua.” “Sasa unafikiri mafanikio yote hayo yanatoka wapi? Ni kwa ibada kama hizi. Na tukifanya pamoja ndio zaidi.” Tunda kimya huku amejawa hofu mpaka vinyweleo vikamsimama. Ibada hiyo ikaanza. Alifuatisha kila kitu alichokuwa akifanya Sadiki. Kadiri muda ulivyokuwa ukienda hapo makaburini, hofu ikaanza kumwisha, akaanza kuzoea hayo mazingira. Baada ya mambo mengi ya hiyo ibada, Sadiki akamwambia wamemaliza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Na mara zote wakitokea huko kwa babu, kila
walipokuwa wakifika njia panda ya
Chalinze, kuna vitu walitupa hapo usiku
huo wa
giza kali, kisha wanarudi Dar.
Tunda alipouliza ni kwa nini,
Sadiki akamwambia kwa kifupi tu,
kuwa wanaita kila mtu anayefika
jijini Dar, kama wanatafuta
nyumba ya wageni, basi wakalale
kwenye hoteli yao. Kuna mtu alifilisika
jijini. Maeneo hayohayo ya Sinza
ambako Sadiki alikuwa na baa,
lakini Sinza Mori. Alikuwa
amechukua mkopo ili kuendesha hoteli
hiyo, aliposhindwa kuiendesha hiyo hoteli na kushindwa kulipa benki, ikapigwa mnada kwa bei ya chini, kwa kuwa Sadiki alikuwa na pesa, akanunua gorofa hilo. Akabadili jina,
akapakarabati zaidi. Akamkabidhi Babu apashugulikie kwa kuvuta
wateja. Babu aliporidhika kuwa amemaliza kazi kwenye hilo jengo ndipo Sadiki
akapafungua rasmi.
Ukweli Sadiki aliwekeza kwenye hiyo hoteli. Alikuwa
ameweka na vivutio vingi kwa wateja. Na kweli walikuwa wanajaza hilo jumba kwa wageni wa kutwa na kulala.
Hiyo ikamtia moyo Sadiki huku akimuhamasisha na
Tunda. Waliona mafanikio ya
ushirikina wanaofanya kwa kupitiae
biashara za Sadiki zilizokuwa zikishamiri haswa. Tunda akatoa ushirikiano wote. Mara moja kwa mwezi walifanya
ibada makaburini makaburini. Wakizika umaskini, mikosi, kulogwa, na mengine mengi Tunda aliyokuwa akimsikia Sadiki akiyatamka wakiwa wanafanya ibada hizo hapo makaburini. Na kwa Babu Chonde hawakuacha kwenda kufanya ibada za kufufuliwa bahati na kutakaswa nyota zaidi.
Siku nyingine maisha yanaendelea jijini kama kawaida. Kuponda raha. Sadiki na Tunda, wala
usingewadhania kuwa wanafanya ibada makaburini. Hayo maisha akayazoea Tunda. Ikawa kitu cha kawaida kwake. Hofu ikaisha.
Tunda akawa na pesa. Akitokea
mahali, utajiuliza mara mbili.
Kuanzia juu mpaka chini, alivaa
vitu vya madesigner wenye majina
makubwa duniani. Viatu vingi alipenda vya Jessica Simpson.
Alisema ndivyo vizuri
vinavyomkaa mguuni kwake na
vinaenda na umbile la nyayo zake. Basi ikawa kazi ya kuvisaka kwa pesa nyingi, ilimradi miguuni amvae Jessica.
Na wakati wote utamkuta Tunda kwenye kiatu cha juu, hata kama ni sendozi. Pochi yake ukiitazama kwa macho, ungejua kuna pesa kubwa iliachwa kwenye hilo duka. Wakati wote ungekuta na kucha safi. Kuanzia za miguu mpaka mikononi. Tunda akawa wa dhahabu halisi na silver za hali ya juu. Akitokea mahali, ungependa kumtizama binti huyo mwenye rangi nyeusi haswa. Mtaratibu, ongea na tizama yake, hana haraka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mwaka wa kwanza na miezi yakutosha ukapita, Tunda na Sadiki wakiishi hotelini, wakiwa wamejaa mafanikio ya namna yao. Mapenzi kwa Tunda yakazidi. Hakuna jinsi ungemtenganisha na Tunda, Sadiki akaweza. Baada ya hiyo nyumba waliyokuwa
wakiilipia kujaa vitu alivyotaka
yeye mwenyewe Tunda, Sadiki akiwa
amegharamia mapesa mengi kuvitoa nchini
Arabuni ambapo wangeweza kupata nchini
hapo kwa bei nzuri, Tunda akakosa
sasa sababu ya kuendelea kuishi
tena hotelini.
Kontena
kutoka Arabuni ilishusha chumba cha
kama alivyotaka yeye Tunda alivyochagua walipokuwa nchini Arabuni. Kuanzia mapazia, kitanda, makabati
makubwa na dressing tables.
Viti vya hapo chumbani na vioo vyake. Na sebule ikawa hivyo hivyo. Hawakukosea hata mapambo. Walimletea kama alivyochagua kule, na vikawa vimefungwa na
vilifika vizuri, vikiwa
hakuna kilichoharibika. Akamtaka wahamie kwenye hiyo nyumba ambayo Tunda hakuta kabisa kuhamia na Sadiki.
Tunda alikuwa akimtii katika kila kitu, kasoro katika hilo na baadhi ya vitu fulani alivyokuwa amevikataa tokea mwanzo kitu kilichomshangaza sana Sadiki aliyekuwa amehakikishiwa na babu kuwa amekwisha kumtengeneza Tunda. Tunda akawa akienda peke yake nyumbani kwake. Sadiki akimtaka, wanakutana hotelini. Hilo likazidi kumkera Sadiki aliyehisi kwenye hilo, uganga wa babu umeshindwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mwanzoni Sadiki alimlalamikia
babu Chonde ugumu anaopambana nao
kwa Tunda. Babu alitaka awe anakwenda naye kuaguliwa, lakini haikuwahi kuwezekana. Tunda hakuwa
akitaka kabisa kuongozana naye sehemu yeyote na alikuwa mbishi kwa kila jambo. Alimwambia akitaka mambo yaende anavyotaka yeye basi akazane
kumshawishi mpaka afanikiwe
kumpeleka Tunda kule kwake. Siku Tunda amekubali kwenda na Sadiki Handeni, akala chakula na kulala zaidi ya masaa 8, mengi yaliendelea akiwa usingizini. Haikuwa shibe iliyomfanya alale. Chakula chake kiliwekwa dawa, ndipo akalala na kufanyiwa mengi. Alipoamka, alikuwa ni kama amepokonywa hiari yake, akawa mtumwa wa Sadiki. Hakuna aliloambiwa na Sadiki, akabisha tena isipokuwa baadhi ya hayo masharti. Alibadilika akawa mtumwa wake. Ila mapenzi ya Sadiki
kwa Tunda ndiyo
yaliyomfanya kumtunza vizuri.
Hakuwahi kumnyanyasa japo Tunda
hakuwa anajielewa.
“Mbona bado kuna ugumu napambana nao?” Sadiki alimlalamikia babu kwenye simu. “Nini tena?”
“Swala la ndoa, mtoto na kuishi naye
nyumba moja! Ni mwaka wa pili huu,
tunakutana hotelini tu! Ameshindwa
kabisa kunikaribisha kwenye nyumba ambayo hata mimi nimeshiriki kununua vitu! Na maanisha kwa kuchagua kabisa!” Sadiki aliendelea kulalamika. “Nilikwambia kama upo
tayari, tumfunge kabisa ufahamu wake,
ukakataa. Hiyo nafasi ndogo uliyoacha,
ndiyo inampa mamlaka. Huyo binti ana
nyota kali sana Sadiki.” “Sasa nitafanya
nini?” “Nakuachia wewe mwenyewe. Lakini
ukitaka nimtengeneze, uniletee kwa siku 7 tu. Niachie kabisa. Mpaka unakuja kumchua huyu, hakuna utakalomwambia akabisha
tena. Na ukifanikiwa kumuweka ndani huyo
kama mkeo, hakuna atakayeweza kukushika
tena. Utakuwa habari nyingine mjini.” Hilo likamuhamasisha Sadiki.
Kummiliki kabisa Tunda! Awe mkewe kabisa na amazalie watoto, ni jambo alikuwa akilitamani sana. Lakini hakutaka amfanye mjinga kabisa! Napo ikawa
ngumu. Alipenda vile
wanavyoweza kutoka, kusafiri na
kuzungumza na Tunda mambo yao.
Akajua Babu akimtengeneza
zaidi, anaweza kuwa mjinga, akakosa hata rafiki na mapenzi yakaisha.
Sadiki akaona
amjaribishe kwanza, kabla
hajampeleka kwa babu kwa siku
hizo saba amtengeneze. Akampigia
tena simu Tunda. “Ani
mama, upo wapi?” “Nipo tu nyumbani.
Unataka nije?” “Kwa nini mimi nisije
huko?” Tunda kimya. “Eti Ani, mama watoto!?” “Tulikubaliana tusizae
Sadiki.” “Hata kamoja kakuunganisha
undugu!?” Tunda akaanza kucheka.
Sadiki hakushangaa. Huwa anacheka hivyo hivyo bila jibu la hapana au ndiyo.
“Nina hamu na wewe Sadiki! Leo utakuja tulale?” Sadiki akajua ndio amebadilisha hoja, hataki. “Nitakuja. Lakini
inabidi tufikirie jinsi yakuhalalisha Ani. Mama Amini ameanza kulalamika. Sionekaniki nyumbani. Lakini akijua yupo mwenzake, atatulia. Naona swala la ndoa sio baya. Ndoa zina baraka zake mama. Halafu utajuana na mwenzio. Mtapanga mambo pamoja. Itakuwa rahisi.” Tunda akanyamaza. “Ani!?” Sadiki
akaita. “Nakusikiliza.”
“Umeamua nini sasa?” “Labda tuache
kulala pamoja usiku, tuwe tunakutana mida ya asubuhi au
mchana. Usiku uwe na mama Amini. Na
safari za hapa na pale tupunguze. Hizo
ndizo zitakuwa zikimtia wasiwasi. Na
swala lakuongeza mtoto mwingine, naona
ubakie na hao hao sita wa mama Amini.
Usiongeze mtoto mwingine.” Sadiki
akakata simu, na kumpigia simu babu kumtaarifu kukubaliana na wazo lake.
“Nitamleta
kwa hizo siku saba. Tafadhali usimfanye
akawa kama tahira. Atakosa maana. Sitaki
aje kuwa mtu wakumsaidia tena.
Ninachotaka ni awe chini ya himaya yangu tu. Afanye kile ninchotaka mimi. Kuishi
naye, ndoa na watoto. Basi. Ila awe anajielewa. Tafadhali sana babu Chonde.” “Usijali. Wewe mlete kwa huo muda tuliokubaliana. Ukija kumchukua utaona mwenyewe. Tena tunaweza
kufunga ndoa huku huku.” “Hapana. Nataka
wajuane na mwenzie. Iwe ndoa
inayotambulika na kila mtu. Nampenda
sana Ani. Nataka watu wajue ni mke
wangu, na aheshimike hivyo. Kwa hiyo
nataka harusi kubwa.” “Sawa.” Babu akakubali bila
shida, Sadiki asijue hila nyingine ya
babu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni kweli
babu Chonde alikuwa mganga wa Sadiki wa
muda mrefu. Hata mke wake mkubwa walikuwa wakifahamiana. Lakini alipompeleka Tunda na Sadiki kuanza kufungukiwa mambo yake, tamaa ikamuanza babu Chonde. Kwanza na yeye
alitafuta jinsi ya kunufaika na huyo
Tunda ambaye walijiambia anabahati ya
pekee. Pili, kule kuchanganyikiwa kwa Sadiki, akimtaka asimuharibu Tunda ili awe na akili zake, babu Chonde akajua kuna analonufaika nalo zaidi Tunda akiwa kwenye akili zake. Na Sadiki naye hakuacha kumsifia Tunda kwa babu. Akimwambia ni bora kuliko mke mkubwa.
Tamaa ikamuanza babu. Kila Sadiki alipokuwa akienda na Tunda, alitamani na yeye apate bahati japo yakulala na Tunda. Anafanyaje? Ndipo akazua hizo siku 7 za kumuagua Tunda peke yake, Sadiki akiwa hayupo, ili aweze kufanya analotaka kwa Tunda akiwa ameteka ufahamu wake. Iwe kwa kumlaza au kumteka ufahamu kwa kujibadili yeye kama Sadiki na Tunda kulala naye kwa hiari yake akijua ni Sadiki ili babu naye afaidi ya Sadiki. Babu akaandaa mazingira hata kwa wakeze, kwa siku hizo 7 atakazokuwa na Tunda, ikabakia kusubiria Tunda aletwe.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sadiki aliaga kwa mkewe kuwa anasafiri kikazi, akahamia hotelini kwa Tunda ambaye alijua watatengana kwa siku 7. Kula, kulala ni hapo hapo hotelini. Kazi ilikuwa ni mapenzi tu. Walikaa siku mbili hapo ndani, ila mida ya usiku walikuwa wakitoka kwenda kwenye kumbi za starehe. Wote wakiwa
wamependeza, usingeweza kusema
Sadiki ni baba wa watoto 6, kwa
mkewe. Ujana ukarudi,
Sadiki anayekimbizana na Tunda
kila mahali kwa starehe,
akabadilika haswa.
Hata uvaaji alibadilika, akarudi kuwa kijana angalau aendane na Tunda. Na Tunda ndiye aliyehakikisha anabadilika na kupendeza. Kila alipokuwa akijinunua nguo, alimnunulia na yeye.
Akambadilisha kabisa Sadiki. Badala ya kuvaa masharti ya vitambaa vya ajabu, Tunda akaanza kumnunulia nguo za kisasa na viatu vinavyoendana na suruali alizokuwa akimnunulia. Sio raba alizomkuta akivaa.
Usiku wakuamkia siku ya tatu akamwambia Tunda kuwa wanakwenda kwa babu. Lakini hakumwambia kama anakwenda kumuacha kwa siku zote hizo saba. Kwani Babu alimwambia Sadiki, atamfanyia dawa Tunda, wala hataelewe kama Sadiki hayupo naye, au hata asijue kama amekaa huko kwa siku zote hizo 7. Alimwahidi
siku atakayokwenda kumchukua,
atajua ndio siku hiyo hiyo
waliyokuwa wamekwenda.
Tabia yao yakufanya dawa kwa babu,
matambiko ya kila
wanapoelekezwa na babu. Kafara na
sadaka walizokuwa wakitumwa watoe na
huyo babu, Tunda alishazoea. Wala hakuwa
akibisha tena. Alipomwambia
wanakwenda Handeni, kesho yake
wala hakuuliza maswali mengi,
asijue anasubiriwa kuwa kitoweo cha babu kwa siku 7. Na kwenda kuharibiwa akili ili akirudi awe kama mjinga kabisa kwa Sadiki. “Tunaondoka ngapi?” Akauliza Tunda bila wasiwasi. “Mapema sana. Nataka tugeuze mapema, ikiwezekana chakula cha usiku tuje kukila hapa hapa Dar.” “Sawa.” Tunda akakubali.
Ila akaona usiku huo ukawa wa tofauti. Sadiki hakutaka watoke, na wakati wote walitaka wawepo hapo kitandani kama wanao agana. “Kwani kesho umeamua kurudi kwa mama Amini? Unataka ukalale kwake?” Ikabidi Tunda aulize. “Ni vile hutaki tu na unafanya mambo kuwa magumu. Mngefahamiana ingekuwa rahisi sana. Na ratiba zingeeleweka kuwa nipo wapi na ninafanya nini.” Hapo Tunda akanyamaza na kulala kabisa.
A |
subuhi
ya saa 10, Sadiki alimuamsha ajiandae. Akiwa
bafuni, Sadiki akamfuata, akaomba penzi.
“Nilifikiri unataka tuwahi!” “Safari ina
mambo mengi mama. Acha tuondoke tukiwa tumeridhishana.” Tunda akacheka.
Wakatumia muda wakutosha tu hapo bafuni, ndipo wakatoka na kujiandaa kwa safari. Walitoka hapo bado giza nje. Kwa kuwa wote walikuwa wamechangamka tu, zikaanza stori. Sadiki akatoa gari hapo hotelini, Mikocheni B taratibu tu wakiwa wametulia na mipango ya kawaida.
Tunda alijawa na furaha, asijue kinachomsubiri
mbeleni, wala Sadiki akiwa hana
hata habari na hila ya babu. Walipofika mataa ya Ubungo, wakiwa wanakata kona kulia ili kuliacha jiji la Dar, kuelekea Kibaha, mbeleni kwenye mataa ikiwa imewaka taa nyekundu. Kuzuia magari ya upande wao kuelekea Buguruni. Kwa kuwa yeye alikuwa anakata kulia, hakusubiri taa ya kijani. Alipofika pale akakanyaga mafuta zaidi kukata kona. Lori la kokoto lililokuwa linatokea Manzese kwenda upande uleule na wao waliokuwa wakielekea kama Kibaha, ikiwa imeruhusiwa na taa za kijani,
dereva alikwisha ziona tokea mbali
akawa anakanyaga mafuta kwa nguvu kuziwahi kabla taa hazijabadilika, aliigonga hiyo gari ya Sadiki iliyokuwa imeingia tu barabarani, ile gari ilirushwa kama kitenesi kwa kuwa zote zilikuwa kwenye mwendo kasi.
Gari aliyokuwa anaendesha Sadiki ikawa kama inapaa mpaka ikatua ndani ya mtaro mkubwa upande wa pili. Kilikuwa kitendo cha sekunde chache, chakustua na kuogopesha sana. Dereva wa Lori alishuhudia akaona vile gari ilivyokuwa ikirushwa. Alisimama mbele kidogo, lakini gari ilipoingia tu mtaroni, kimya kwa sekunde
kadhaa yule dereva akakanyaga mafuta
na kuondoka pale bila kutaka kujua kulikoni ili asikamatwe kama ameua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda amepata ajali mbaya
sana akiwa na mume wa mtu, akiwa anakwenda kwa mganga wa kienyeji. Mengi yalipangwa juu yake. Lakini safari imeishia mtaroni. Nini kimempata Tunda safari hii? Endelea kufuatilia.
Sehem ya 11 tafadhar da Naomi siion
ReplyDelete