Love At First Sight - Sehemu ya 65.
Chezo alimuacha
Pius haamini. Alijuta hata kwa nini alimtafuta. Akabaki amevurugikiwa
hajui hata awaze kipi! Ujumbe wa Raza nao ukaingia na kumtoa kwenye mawazo ya
Chezo. ‘Kama majukumu yamekubana, usiwe nawasiwasi, naweza tu agiza
matunda, nitakula vizuri nyumbani, nikitoka.’ “Mimi ndio nionekane sijali!” A kajiwazisha Pius na
kurudisha ujumbe. ‘Nakuja sasahivi.’ Ndipo akatoka. Nakumfuata tena mpaka ofisini kwake na
kumchukua.
Raza alimuona
wazi amebadilika tokea anaingia ofisini kwake. Kikamnyima raha. Akahisi anaanza
kulemewa kutoka naye kwa chakula cha mchana kila siku. “Si unajua mimi
nitakuwa sawa tu hata ukishindwa kuja kula na mimi mchana? Usilazimishe
kuja kama umebanwa na majukumu kazini. Huna sababu ya kufanya hivyo.” Ikabidi amwambie
kabla hajaondoa gari. Kimya. Huku akijiambia mbona Chezo yeye alikuwa akikutana
na mkewe kila siku mchana! “Wasinichezee akili. Hata mimi naweza.” Akajiambia
lakini ukweli wawili hawa si sawa. Pius anamajukumu mazito sana ya kiofisi. Hapo
amevurugwa tu, hawezi kufikiria sawasawa.
“Mimi naweza
kurudi tu ofisini nikaagiza waniletee matunda ofisini.” Raza akaweka msisitizo.
“Nataka twende ukanionyeshe hiyo nyumba mnayojenga, maana jioni ya leo
tunamiahadi na huyo contractor.” Raza akatulia baada ya kusikia, ‘mnayojenga’,
halafu na sura ambayo kama imejaa hasira! Akatulia na kumpa maelekezo ya
awali. Akatoa gari, Raza kimya ametulia kitini.
“Najiuliza, hivi
ikitokea nafukuzwa kazi sasahivi. Biashara zote zinakufa,
bado utabaki na mimi?” Raza akashangaa sana hayo yanatoka wapi ila akajikaza na
kumjibu. “Nilifikiri tumekubaliana kuanza upya! Na kwamba sasahivi
tumebaki mimi na wewe kama ulivyosema! Kwani kuna nini tena?!” “Kwamba tunabaki
wote kwa sababu tumejikuta tu pamoja, kosa la ndoa lilishatokea,
inatubidi kubaki tu, au kwa sababu kuna mapenzi?” Akamuona anaanza
kupandisha hasira.
“Maana unaweza
kuta hata hii ndoa inageuka kuwa mzigo! Mwanaume siye uliyekuwa ukimtaka.
Nikimaanisha si mwanaume wa ndoto zako. Umekwama kwenye ndoa,
ishatoa matokeo ya watoto, na pengine kuna maslahi mengine yanayo kubakisha.”
“Ukimaanisha nabakizwa kwako na pesa zako?!” Raza akamuuliza kwa kumshangaa
sana, asijue mwenzie anajifananisha na Chezo vile alivyo, na
maneno machungu aliyompa.
~~~~~~~~~~~~~~
Pius japokuwa
anapesa na alikuwa kwenye ofisi nzuri wakati akikutana na Chezo lakini Chezo alimtisha.
Alikuwa na umbile la kiume japo urefu hawakupishana. Amejazia hata kwenye shati
alilokuwa amevaa alionyesha amejenga misuli. Safi utafikiri ni mkurugenzi
aliyekuwa ameacha koti la suti kwenye gari na kwenda kukutana na Pius. Halafu
akajibeba vizuri kwelikweli! Bila paniki wala hofu na kuweza kumuachia
maneno yaliyobaki yakimsumbua Pius.
Mwizi akamtisha mwenye mali mwenyewe, Pius akajiona kipanzi. Kwamba
Raza kurudi kwake ni kama anamuhurumia tu. Akamuona Chezo ni bora kuliko yeye!
Japokuwa mwishoni alitumia ubabe lakini wazi kwa hoja alimshinda.
~~~~~~~~~~~~~~
“Ni nini tena,
Pius?! Mbona mwanzo uliosema ni kama tena unaanza na manyanyaso?” Kidogo
akashituka na kujua amepitiliza. “Si kwamba nakunyanyasa, ni
kutaka kujua kwa ajili yako wewe mwenyewe. Sitaki uje uache maisha yako huko,
unakuja kujipunja kwangu.” “Maisha niliyoishi hayakuwa sahihi mbele za
Mungu, Pius! Nimebadilika kwa kupenda kwangu nikitaka kuishi maisha matakatifu
nikimtegemea Mungu. Ya kale yamepita, Mungu ameniahidia mapya.
Tafadhali naomba na wewe unisaidie sio kunirudisha kwenye maisha ya
nyuma.”
“Chochote
nilichokuwa nikifanya zamani, nimekusudia kubadilika! Nimeacha
ushirikina na mengine yote.” Asijue wala tatizo sio uchawi ni Chezo
aliyekwenda kumtafuta yeye mwenyewe.
“Sasahivi nina
amani na utulivu nafsi kwangu.” “Huna majuto?” Raza akashangaa sana. “Najutia
nini!?” Pius akababaika haswa ila akionekana ameshapoa kama aliyejishitukia
kwamba amempandishia hasira mtu ambaye hata hakuwa na wazo!
“Sitaki uishi na
mimi kwa kunivumilia tu.” “Kuna tatizo gani nikikuvumilia
wewe mume wangu!?” Akamuuliza vizuri tu na kumfunga mdomo. “Maana ni kama
ulisema sasahivi tumebaki mimi na wewe! Sasa kama tumebaki wawili, si
ndio tunabebana katika kila hali!”
“Na tafadhali
swala la nyumba yangu lisikunyime raha Pius. Nimejitahidi kwa juhudi zangu
nimefika hapo nilipofika.” “Sema juhudi zenu!” Raza akatulia. Pakatulia
kwa muda akiendelea kuendesha. Kimya.
“Hapa niende
wapi?” “Naomba nirudishe tu kazini, Pius. Hili jambo nafikiri litatukosanisha.”
“Kwa hiyo hutaki niingilie kumbukumbu yenu? Unaona kama mimi nitakuwa mvurugaji
tu?” Raza hakujibu kwenye hilo, akamuelekeza mpaka wakafika.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakashuka
garini, akaanza kuzunguka akishika kila mahali. Kimyakimya Raza akifuata nyuma.
Akazunguka mpaka akamaliza. Wakarudi garini.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kwanza nakupongeza.
Umejitahidi sana.” Raza kimya. Akamuita. “Raza, nimekupongeza!” “Asante.”
“Lakini nimeshika ukuta, wazi unaonekana mchanga ni mwingi kuliko
cement.” Akaanza kukosoa. Raza kimya huku wakirudi ofisini, maana muda
ulishaisha hawakuweza kupita kula.
Akalalamikia
ujenzi wa hiyo nyumba kuanzia msingi mpaka ilipofikia, utafikiri anayo shahada
ya fundi nyumba! Raza kimya ila akihisi tatizo ni Chezo tu
kuhusika kwenye hiyo nyumba. Kimya hakumjibu mpaka anamshusha ofisini. Ule moto
wa kuanza upya ukawa umeshamwagikiwa na tui la nazi jikoni, na kuzimisha.
Wakapoa tena kama waliopoteza dira.
~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi nyumbani
usiku akamkuta Raza jikoni akimalizia kusafisha. Kwa asili Raza alikuwa msafi
sana. Huacha jiko safi ndio anakwenda kulala. “Nimemchelewa Polla?” “Muda si
mrefu. Pole na kazi.” “Na wewe. Vipi hapa?” Akauliza huku akitafutia samaki
nafasi kwenye friji.
“Ni nini hicho?”
“Samaki, alileta Chezo ofisini kwangu.” Alishituka Raza karibu aangushe
sahani, ila akaidaka ikimponyoka mara kadhaa mikononi mwake. Tumbo likaanza kuvuruga.
Pius akajua kabisa ameshituka, akatoka hapo kwenda mezani alijua chakula
kinamsubiria. “Nashukuru kwa chakula.” Akamsikia akishukuru huko mezani. Lakini
alishindwa hata kujibu! Akaweka sawa hapo jikoni, akapitiliza juu chumbani
kwenda kuoga.
Akiwa bafuni
ndio kama akili ikaanza kumjia kuwa mumewe amekutana na Chezo, ndio maana alitibuka
mchana. Wasiwasi walichozungumza ukamuingia, ila hana wakumuuliza. Chezo asingethubutu,
na mumewe hivyohivyo.
Nyumba ile
ikaanza kuwa tatizo. Akajua itabaki kuwa tatizo kwa sababu
imebeba kumbukumbu za Chezo. Akabaki akiwaza hajui chakufanya. Ni jasho
lake na kweli alitaka angalau awe na kitu chake kinachotokana na jasho
lake. Lakini napo akakumbuka jinsi mumewe alivyokuwa akiikosoa! Ikakosa
raha kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati akijipaka
mafuta Pius naye akaingia kuoga. Raza hakumsemesha hapo kwenye chumba cha bafu.
Akavaa na kutoka akajiwahi kitandani. Pius naye hakukawia kama aliyekuwa
akimuwahi. Alipojiweka tu kitandani, Raza akamgeukia.
“Naona tu niuze
kile kiwanja na ile nyumba ilipofikia, nikaanze kujenga upya kwingine. Hata
hivyo kama ulivyosema, mchanga ni mwingi kuliko simenti.” “Nilikuwa na contactor
huko jioni hii ndio maana nimechelewa. Hata yeye ameona jinsi ilivyojengwa vibaya.
Hata msingi wenyewe unaonekana haupo imara.” Akaanza kukosoa
tena. Raza kimya akisubiri hitimisho.
“Kwahiyo kesho
wanaanza kuibomoa.” Raza akashituka akahisi roho inataka kutoka. Akakaa
kwa mshituko bila kutarajia. “Yote!?” Akauliza kwa mshangao wa wazi kabisa.
“Mpaka msingi. Kwanza pale ilipo tumeona sio sehemu nzuri. Ataisogeza kabisa
wajenge sehemu nzuri ili kuwepo na bustani nzuri na ya kueleweka. Nafikiria
mpaka kupata uwanja mzuri kuja kuweka bwawa. Hata yeye ameona ni wazo zuri, ipo
karibu na bahari, uchimbaji wa pool hautakuwa shida. Tutapata maji kwa rahisi.”
Raza kimya mapigo ya moyo yakiendelea kwenda sivyo.
“Wanaanza kazi
mara moja, wameniahidi ndani ya miezi 6 itakuwa tayari hata kuhamia. Au kuna kumbukumbu
unatunza pale?” “Ni jasho langu ndio maana nimeshituka Pius! Lakini
nashukuru kwa kunihangaikia.” Akarudi kujilaza akiwa amenyongea moyoni.
Hakutaka hata kuzungumza jingine akaona alale tu.
“Hela nzima ya
ujenzi nitaihamishia kwenye akaunti yako, tutakuwa tukimlipa kwa awamu.
Nitakuonyesha mkataba wake na hiyo ramani mpya. Na hii sio ya kwenda kusimamia
kila siku. Ndio uzuri wa contractor.” Hapo kidogo akatulia. Kuna
leo na kesho. Akianguka na kufa Pius gafla na nyumba
kambomolea! Hapo kidogo akaona bora pesa itakuwepo, tena kwenye akaunti yake.
Mapigo ya moyo yakaanza kutulia. “Nashukuru. Asante.” Akajua wazi amepoa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nimezungumza na
Andy, ijumaa hii tukitoka kazini, tunaelekea Dodoma, nyumbani kwao. Tulimalize hili
kabla hawajarudi hapa Dar. Au unampango mwingine?” “Hamna. Nashukuru
kunisindikiza.” “Pia itatupa mapumziko mengine. Nilipata wakati mzuri na wewe
tulipokuwa Mauritius. Natamani tuwe tunajitengenezea mazingira kama yale mara
kwa mara. Ikawa sasa kama anayempuliza baada ya kumng’ata.
Raza akatulia
akiwa na mengi yanayoendelea kichwani mwake akijaribu kurudisha mudi. Kubomolewa
nyumba aliyohangaikia kwa kiasi kile! Bado alikuwa akijaribu kuingiza akilini, huku
akijilaumu kumwambia kama na Chezo alikuwa akisimamia.
“Au unataka twende na kugeuza?” “Ningependa wakati
mwingine mzuri. Tunakwenda na watoto?” “Inabidi na wao wakamuone kaka yao. Si
ni sawa?” “Hamna shida. Nashukuru.”
Wakapanga tena mipango
wa hiyo safari ya Dodoma. Siku ya kwanza ilikuwa ni ya kwenda kuomba msamaha
kwanza, wawaache watoto hotelini. Ndipo siku ya jumamosi waende na watoto wao
hapo kwa kina Andy. Hilo likakaa sawa.
Lakini kulikuwa
na uzito usiku huo, hakuna hata aliyekuwa na hamu ya mapenzi. Walilala kila mtu
akiwaza lake. Kale kahali kafungate, upepo ukakapitia,
wakarudi kulala kama wanandoa wa kongwe, kavukavu bila hata kugusana.
~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi ndipo
akasikia chuchu zinashikwa taratibu. Akiwa usingizini hakujua kama ni mumewe,
akageuka upande wa pili akidhania ni ndoto. “Usinichukie Raza, na kunikataa.
Nia yangu ni kujenga chetu, tena kizuri chenye hadhi.” Ndio Raza kutoka
usingizini sasa baada ya hayo malalamiko. “Pole, nilikuwa nimelala nikadhania
ni ndoto.” Akageuka vizuri.
“Na
sijakuchukia.” “Unauhakika?” “Sema nikushituka tu. Ile nyumba nimehangaikia
Pius! Nishaiona ikiwa imeshaisha kabisa. Kusikia inabomolewa si kitu kidogo!”
“Sasa tutakuaje
na kitu chetu, au mwanzo wetu na Chezo katikati yetu?” Hapo la moyoni
likawa bayana. “Umeichukulia vibaya tu. Chezo alifanya kama mfanyakazi
tu. Kusimamia. Hajaweka pale hata shilingi yake!” “Kuna kujenga kwa kujitolea
kwa hali na mali. Yeye amejitoa kwa hali, wewe mali.
Sasa mimi hapo nipo wapi?”
“Na ndio maana
wewe unajeuri hata na hii nyumba Raza. Umenikuta nikijenga. Tulikuwa tukija
wote hapa kipindi ikijengwa. Maua yote kwenye hii nyumba na ukoka ni wewe
ndiye uliyekuwa ukileta hapa hata kabla ya ndoa yetu. Unahaki na jeuri
ya kusema hapa ni kwako pia hata kama hukuwekeza pesa ya ujenzi wa hii
nyumba kama jengo, lakini unamchango wako hapa. Lakini Kule itabakia ni wewe
na Chezo daima! Ila kama itakuumiza, basi, nipo tayari niache
nisikuingilie.” Asubuhi hiyo alionekana mnyenyekevu kama si yeye!
Lakini Raza
alijua wazi, akitaka amani humo ndani na mengine yaendelee vizuri,
hiyo nyumba kubomolewa ndio itakuwa garama ya kulipa. Akamua anyamaze.
~~~~~~~~~~~~~~
Muda wake
ulikuwa umeshaisha, alamu iliita ikabidi kukurupuka na kwenda kusamdia Polla,
awahi shule na kuandaa kifungua kinywa cha mumewe. Pius akaachwa bilabila hapo
kitandani. Huyo Raza akawa hagawanyiki na hesabu ikakaa sawa. Kazini
anahitajika kwa asilimia zote, nyumbani mambo yote yanamtizama yeye,
na kitandani! Hapo ikabidi Pius awe mpole. Akajituliza kwa kujipoteza mawazo
kwenye hili na lile akisubiria na yeye alamu yake, atoke kitandani, siku ianze.
Kila ‘Samahani’,
Hubeba Gharama.
Kuomba msamaha si
maneno matupu. Ni sadaka ya moyo inayotolewa kwa unyenyekevu.
Ni safari ya kuvuka daraja la kiburi, ukiachilia mizigo ya hasira
ili kubeba uzito wa ukweli. Walifika Dodoma jioni mapema tu kabla giza halijafukuza
mwanga, maana waliwahi kutoka ofisini. Wakaelekea hotelini kuacha watoto wao
ndipo wakaenda kwa Andy.
Wakakuta
wameandaliwa vilivyo. “Sisi tulijua mnakuja na watoto kama Pius alivyosema!
Mpaka pakulala tumewaandalia nyinyi na watoto.” “Tumekuja nao ila tumewaacha
hotelini. Tuliona tuje sisi kwanza, tuzungumze.” “Karibuni.” Wakaingia ndani
maana Andy ndiye aliyekwenda kuwafungulia mlango baada ya kusikia geti
linafunguliwa akiwa amembeba Ayvin. Walituma dereva wao kwenda kuwapokea.
“Nipe huyo
nimsalimie.” Ayvin akamkataa kabisa baba yake akabaki amejificha begani kwa
Andy akimng’ang’ania. “Hapo ndio ujanja wote humuisha. Ila kwa kuwa
hajiwezi kwa utundu, mkikaa kidogo ataanza kuwachungulia mwishoe atashuka tu
hapa yeye mwenyewe aanze kuzunguka. Mpeni muda. Karibuni ndani.” Wakaelekea
mpaka sebuleni alipokuwa amekaa Mina na Ayan.
Mina alikuwa
ametulia kimya walipoingia, akasimama na kuwapa mkono akiwakaribisha. “Meza
imejaa vyakula tukijua mnakuja na watoto!” “Tumekuja nao ila tumewaacha
hotelini, ili sisi kwanza tuzungumze.” Andy akakaa na Ayvin begani
ametulia kama sio yeye.
“Mbona huyo
kwenye video anaonekana mtundu sana?” Pius akauliza akionyesha wazi anatamani
kumshika mwanae. “Ujanja wake unaisha akishasikia hodi. Anatulia kama si yeye
mpaka mgeni aondoke. Eti Ayvin?” Andy akamchungulia pale alipojificha. Akazidi
kumng’ang’ania. Mina kimya kama Raza.
“Basi wewe Ayan
njoo uchukue zawadi yako. Dady amesema unapenda vitabu, si ndio?” Akakubali
akitingisha kichwa. “Basi Poliny amekutafutia vitabu vizuri sana, utapenda.
Njoo.” Akawa anasita huku akimtizama mama yake kwa hofu. “Huyo,
hapo hawezi sogea. Anamuogopa sana Raza.” Mina akaongea maana
walishangaa Ayan ameshindwa kabisa kusogea japo alionekana amependa
zawadi.
“Raza alikuwa akimpiga
sana Ayan ndio maana anamuogopa.” Mina akaongea kwa jazba. “Sio sana!”
“Unabisha nini wakati hata Polla aliniambia na kumwambia babu yake kuwa ulikuwa
ukimchapa na kumnyima maziwa? Labda useme kama Polla ni muongo
ila na Mamu naye pia alishasema unamchukia mwanangu na unampiga SANA
japo mtoto mwenyewe ni mkimya.” Mina akaongeza kwa hasira.
“Ndio maana
nimekuja kuomba msamaha.” “Wakutaka kumuua, sawa. Lakini jua ashajua humpendi,
anakuogopa.” Kidogo pakatibuka kama maziwa yaliyokuwa yakichemka
taratibu gafla kumwagika na kutibua jivu. “Itachukua zaidi ya vitabu
kuwaamini nyinyi wote wawili maana wakati mwingine na wewe Pius ulikuwepo
wakati mkeo akimpiga mwanangu.” “Hajawahi mpiga mbele yangu.” “Basi jua
Ayan anajua kama na wewe ulikuwa ukijua kama mkeo alikuwa akimtesa
na hukumtetea. Ndio maana kama umegundua alikuwa akikupenda sana
zamani. Akaja kukubadilikia. Siku hizi akikuona mahali anakukwepa kwa hofu,
hakukimbilii kama zamani alipodhania ulikuwa kimbilio lake.” Mina akawa
ameshapandisha.
“Ayan nenda
kasome vitabu vyako ndani.” Baba yake akamtoa hapo. Hakuchukua hata sekunde,
mtoto akakimbilia ndani kama mshale. Gafla pakapoa hapo, wakawa kama wamepoteza
dira. Kimya. Andy akajisogeza nyuma na mtoto begani, akajiegemeza kwenye kochi,
akatulia. Kimya kwa muda.
Ukifunika Kosa
Leo, Kesho Litakuja Kama Dhoruba Kali
Ni kweli siri
ya makosa ni kama tu. Mwishoe hutoka hata ukiziba kila ufa. Muda
mfupi uliopita, kabla na hata walipokaribishwa ndani ni kama kulionekana maisha
yaliweza kuendelea. Lakini kumbe ndani bado kulikuwa na madonda mabichi
yaliyokuwa yamefunikwa na ngozi kavu kama kovu.
Pakatibuka kwa machungu ya dhambi ya nyuma ambayo ilionekana ndogo
na kushindwa kutubiwa. Walikuja na la uuwaji, kumbe kuna mengine
alifanyiwa mnyonge Ayan sirini, Mungu akaona na hilo liwekwe mwangani.
Pius alikusudia watoke hapo wakiwa
wameyamaliza. Akaangalia ile hali, akaona yeye ndio aanze maana ni kama Raza
alinyong’onyea, akashindwa jinsi ya kuendelea kuanzia hapo.
“Kuna makosa
mengi yametokea, naomba nianze na kubwa na la kwanza, swala la mtoto. Ukiangalia
kwa makini na kufikiria tokea mwanzo, mimi ndiye niliyekosea tokea mwanzo.”
Akaanza Pius. “Mimi ndiye niliyekosea kuanzia kutungwa mimba yake mpaka
anarudishwa baada ya kuzaliwa. Kosa moja ni lakuficha ukweli wa mambo,
ilimgarimu Mina na Andy.” “Umeruka Pius. Tafadhali kama umekusudia kuomba
msamaha, omba ueleweke.” Akaingilia Andy.
“Ushikwaji wa
mimba ulitokea wapi?” Akamuuliza na yeye kaka yake kwa ukali. “Ni
kweli.” Pius akakubali kwa kujishusha. “Tokea mwanzo kumpa Mina pombe.” “Na
kuingia kwenye chumba changu na kulala kwenye kitanda changu cha
ndoa, tena takatifu! Uliwezaje Pius?!” Hapo na Raza naye akamgeukia
mumewe vizuri. Makosa yasiyoelezwa hukua kama kivuli
kinachokuandama hata jua likiwaka. Pius alishindwa kuepuka huo ukweli.
“Nimekosa
Andy na naomba tu niwe muwazi. Tulijenga ukaribu na Mina nafikiri hapo
ndipo nilipopitiliza. Nimekosa Andy, naomba msamaha.” Ungemuona Pius
huyu mpaka akawashangaza na wao.
“Na katika hili
hata Raza narudia kukuomba msamaha. Nimekosa mke wangu, naomba na wewe unisamehe.
Kuanzia kabla na baada ya mimba, jamani, sikufanya vizuri. Ningefanya
vizuri hata baada ya kujulikana kama mtoto ni wangu, nina uhakika wote
nyinyi, mpaka wazazi, Raza zaidi, asingefika alipofika.”
“Mimi ndiye
niliyemtia hofu Raza. Nikampuuza mpaka akatishika na
kufanya aliyoyafanya.” “Sema kutaka kuua watoto wangu. Kama kweli
mmekuja kuomba msamaha, ombeni mueleweke msiweke kificho na hapo
ndipo kupona kwa kila mtu. Msiweke lugha ya mafumbo wakati kila
mtu anajua Raza alikusudia KUUA wanangu lakini akakutana na Mungu aliye
HAI. Na kama isingekuwa nguvu za Mungu, inamaana pengine sasahivi nisingekuwa
na mtoto hata mmoja!” Bwana wenye nyumba hao walikuwa wakali!
Raza akapiga
magoti kwa haraka. “Nimekosa Mina. Nimekosa sana. Niliingiliwa na roho chafu
na nakiri niliiruhusu mimi mwenyewe sababu ya wivu tokea mwanzo. Mtoto
wa kiume nimemtafuta jamani, karibu kuchanganyikiwa. Na hapo ndipo
lilipokuwa anguko langu. Nilifungulia milango mingi na shetani akajua udhaifu
wangu, akanitumia.”
“Nisamehe
Mina. Nimekosa na nimetubu. Nimempa maisha yangu Yesu, sasahivi
naishi kwa kuongozwa na yeye.” “Hapo sasa ndio itakuwa pona yako. Maana
hivihivi utajikuta kila mwaka mnarudi hapa kuomba msamaha. Shetani
hanaga mpango wa kukamatwa na kumuachia mtu. Jua atakujaribu tena
na tena maana naona na Mungu naye ameamua humu ndani kuzaliwe madume
matupu. Sasa utashindana na Mungu mpaka lini?”
“Nimeacha kabisa
Mina. Hata mambo ya waganga nimeacha kabisa. Na japokuwa bado watu hawajanisamehe,
lakini moyoni nipo kama nimetua mzigo mzito. Kwanza mimi mwenyewe nilikuwa nikiteseka!
Havina raha na wala havikuwahi nisaidia. Nimekosa Mina. Nimekosa hata kumchapa
Ayan.”
“Sasa hilo ndio kosa
lililokuwa likiniuma sana, Raza. Kumchapa mwanangu asiye na hatia
kabisa! Ulimuonea mwanangu bila sababu! Ukatumia upweke na unyonge wake kumuadhibu
mwanangu. Mtoto aliyekuwa ametelekezwa na wazazi wake! Mnyonge
asiyeweza kujitetea wala kukushitaki kwa mtu, ukamchagua kumtesa yeye, sababu
tu, eti amezaliwa wakiume!”
“Halafu kwa utajiri
wote mliojaliwa nyinyi wawili, kweli kumpa mwanangu maziwa ukawa unaona shida!
Mnamnyima mwanangu chakula kilichojaa ndani kwenu mpaka kuharibika na kutupwa!
Roho mbaya gani hiyo Raza wewe!? Chakula tu!?” Mina akawa ameshakuwa juu haswa.
Hasira.
“Hakika hapo ndipo
uliponiumiza na kunikosea Raza. Lakini huko kumuua mimi
sikujali kwa kuwa nilijua HUTAWEZA, hata uende kwa shetani mwenyewe,
huwawezi wanangu.” Mina akakaa sawa akiwa bado na hasira, Raza kapiga
magoti mbele yake.
“Hakuna mchawi
atagusa mwanangu, akafanikiwa. Ndio maana waliposema wanakufunga
kwa uchawi wakutaka kuua wanangu, nikasema hapo wala sioni
kosa. Ila kuchukia wanangu, ukiwaonea na kuwanyanyasa, halafu na kusambaza
maneno mpaka kumchanganya mama yangu ukimuabisha! Hapo HAPANA
Raza. Bora ukaloge utakavyo ila usimuuwe mama yangu kwa fedheha.”
“Wala na hilo
usiwe na wasiwasi nalo. Watu wananikimbia sasahivi. Huyo Mamu ndio utafikiri
ametumwa kunitesa! Ananitangaza ubaya kwa kila mtu! Mwenzio
nimegeuka kichekesho kwa watu, mpaka ndugu! Ananitangaza ubaya mpaka kwa
wafanyakazi wangu, kwamba mimi nawaloga ndio maana wanakaa pale muda mrefu. Eti
nimewafanya kama msukule. Msichana wa kazi aliyekaa na mimi zaidi ya
miaka 10, ameondoka sababu ya Mamu! Watu wananikimbia Mina! Mimi mbaya.”
Raza akazidi kutokwa na machozi.
“Sasa na wewe
usikubali kujisemea mabaya. Wewe si umempa Yesu maisha?” Akakubali
akitingisha kichwa mumewe akamsaidia kumfuta machozi. “Wewe ni mbarikiwa
sio mbaya. Yakale yote yamepita, wewe sasahivi umekua mpya.” “Kwahiyo
sasa umenisamehe?” Mpaka Mina akacheka.
“Si umesema mwenyewe yakale
yamepita, nimesamehewa? Basi na wewe nisamehe Mina! Tulee wote watoto.” “Na uache kuwapiga wanangu.” “Hata wakikosa?” Raza akauliza akikaa na kujifuta machozi. “Basi hawaji huko kwenu.”
“Nakutania bwana! Siwachapi tena. Wakija nitakuwa nawapa maziwa na
nitakuwa mama mzuri kwao. Hakika nimebadilika Mina. Nilikuwa nimebeba chuki,
sijui kwa nini!”
“Si hata Poliny
mwenyewe alikuwa hawezi kuishi na mimi? Unakumbuka hata kwako alikuwa
akikulalamikia?” “Nakumbuka.” “Sasahivi mpaka yeye anasema eti anakuwa na hamu
na mimi!” Wakacheka. “Kila siku ananitafuta mwanangu na kunijulia hali kitu
ambacho hakikuwepo kwake! Mpaka ananiomba mimi ushauri na kutaka niwe
namuombea!”
“Nisamehe tu
Mina. Nilijichanganya tokea nilipoanza kwenda kwa waganga. Huko ndipo
nilipokwenda kubeba maroho mengine ya ajabu yakawa
yakinipelekesha mpaka kudhuru watu.” “Yameisha. Na kama una shida na
msichana wa kazi wewe niambie. Kuna mtu anatafuta kazi. Alikuwa akitusaidia
hapa kabla sijatoroka na wanangu, sasa nimerudi na huyu, amezoea wanangu
na naona wenyewe tunaelewana kwa kusukumana hivyohivyo, sitaki
kumbadilisha.”
“Sasa yule wa
kwanza amerudi na anashida sana. Ni mdada mzuri, anamcha Mungu na ndiye
aliyenisaidia kunihimiza kuzungumza na Andy kipindi kabla sijajua mumeo
ndio baba mtoto.” Akamtizama Pius kwa hasira.
“Nilikosea Mina,
ila ujue nilipanga nije kukwambia.” “Wewe ni mbaya Pius.
Uliniacha nadhalilika, ukabaki kimya!” “Na hilo natubia. Tafadhalini naomba
mnisamehe. Andy, tafadhali nisamehe. Kwa yote. Kuanzia Mina
mwenyewe mpaka kuzaa naye. Si sawa. Nimekosa.” “Hilo ndilo
nilitaka kukusikia.” “Nimekosa. Na nilikosea tokea mwanzo. Tafadhali naomba
unisamehe.” “Naona na kosa lenyewe limekuja kuwa baraka kwangu.” Akamchungulia
Ayvin pale alipojilaza begani kwake. Alishalala.
Pale Mungu
Anapobadilisha Ubaya Kuwa Wema.
“Ayvin ni mtoto mzuri
sana. Hata wewe Raza, ukimfungulia moyo kwa ukweli, utagundua Mungu
ameleta faraja kwetu SISI WOTE. Amekuwa mpaka dawa kwa mzee Ruhinda bwana! Yaani mzee
Ruhinda anafanya mambo ambayo hata mama anasema hakuwa akiyafanya kwetu! Na ili
usipatwe wivu, jua ni Ayvin tu wala si watoto wa kiume maana Ayan
mwenyewe hamchangamshi babu yake kama huyu.”
“Ayvin ni faraja
na kicheko mpaka kwa Ayan mwenyewe. Kwa hiyo mpe nafasi bila kujali jinsia
yake, kwa hakika utamfurahia. Na hata hili nilimwambia Mina. Kama
tutamkuza hivihivi kwa upendo, kusiwekwe hofu kama mlivyofanya
kwa Ayan. Mkimnyanyasa bila hatia, mkamuingizia hofu kijana
wangu. Mkiepuka hilo kwa Ayvin. Akapewa uhuru wa kuwa vile Mungu
alivyomuumba, basi mjue familia ya Ruhinda kila mmoja atamfurahia. Ni mtoto
mzuri sana. Na si mchoyo hata kidogo.”
“Kwa udogo wake
huyu, ukimpa kitu kizuri, akakipenda. Hata ukimuwekea mdomoni, atatoa na
kumpa Ayan.” “Aisee kweli! Kumbe na wewe umemuona?” Mina akaingilia hakuwa
amejua kama mumewe amegundua. “Kabisa. Mpaka mimi ananishangaza! Huna
kitu ukampa yeye, kaka yake na yeye asipate. Sasa hebu niambie afundishwe hivyo
kuwa dada zake woote, aambiwe nao ni ndugu zake. Halafu akafanikiwa
kwenye maisha. Baada ya miaka 50 kuanzia sasa sisi tukiwa hatupo hapa, si
tutakuwa tunauhakika tumeacha watoto wote kwenye uangalizi mzuri?”
Mpaka Pius akashangaa na kujikuta akitokwa na machozi. Akayafuta kwa haraka
sana.
“Nakushuru Andy. Aisee asante sana.
Nashukuru.” Pius akajikuta akisema hivyo. “Haiba yake si
yakuficha huyu. Ngoja awazoee, halafu akue kidogo muone jinsi tutakavyokuwa tukinyang’anyana.
Ila tu isitokee wakumuharibu akili. Na haya mambo ya MALI hili hata Mina
nimemwambia. Na wewe Raza nakuomba. Acha kufundisha vijana wangu
maswala ya mali zetu. Waache wakue, wajue mali ni za baba na
mama, wao watafute ZAO!” “Nashukuru Andy.” Pius akaongeza.
“Hakika tutawadumaza.
Utakuja kuta tunakua na vijana wasio pambana kwenye maisha,
wanasubiria mali ambazo kwanza si zao na wanaweza hata wasije kurithi
mpaka wanakuwa watu wazima, wanasubiria tu! Tuangalie sisi vijana wa
Ruhinda. Hakuna aliyerithishwa, lakini wote tunapambana. Na
tulipofika hapa, hebu niambie mzee Ruhinda atatupa nini ambacho sisi
hatuna?”
“Hata Pius
ameniambia hivyohivyo! Ni uelewa mbaya shemeji yangu. Nimekoma,
naomba na wewe unisamehe!” “Aisee kwa huyu nitakuwa mkali hata kwa baba
yake. Naomba tusije mchanganya. Ni mtoto mzuri sana. Hajijui
jinsia yake ila anajua watu wanao mzunguka na kuwapenda sana. Hakika sitaruhusu
mtu amchanganye.” Hata Mina ilimgusa. Hakutegemea kwa umbali huo aliokuwa
akiusema. Andy alionekana kumaanisha kutoka ndani.
“Tafadhali
naomba nimshike akiwa hivyohivyo amelala!” Andy akaenda kumpa. “Nimepitwa na
mengi sana.” Pius akaongea kwa kulalamika akimwangalia kijana wake. “Sio sana.
Kuanzia wanarudi mpaka sasa, nimechukua kumbukumbu zake nyingi sana ili
asije bisha baadaye. Ayvin ni mtundu sana aisee.” Wakacheka vile Andy
alivyoongea ila kwa kuvutiwa sio kwa ubaya.
“Mpaka siku ya
kwanza anaanza kutambaa kabisa. Nilikuwa naye, na nilifanikiwa kumpata vizuri
sana kwenye video.” Andy akaongeza. “Tafadhali nitumie kila kitu.” Pius alikuwa
akimtizama huyo mtoto kama asiyeamini, kama ameokota alumasi!
“Aisee amekua! Halafu anamwili!” “Mlaji mzuri.
Hasumbui kula labda akimuona mama yake, napo namuona kama ameanza kubadilika
sio kama zamani akimuona mama yake, hataki kula kabisa anataka kunyonya tu.”
“Itakua kukua.” Pius akaongeza. “Na michezo mingi. Wakati mwingine anakuwa
amezidiwa michezo hata hajui kama nipo mahali. Na Andy akiwepo ndio kabisa!
Akili zinakuwa kwa Andy tu. Anajua yeye ndio anampatiliza.” Mina
akaongeza. Pius akamuweka kifuani vizuri akaanza kumpapasa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alikuwa msafi,
ananukia vizuri, utajua yupo na matunzo mazuri. Kwa asili Mina alipenda
kuvalisha wanae mpaka walikuwa wakimsema hana akili ya matumizi ya pesa.
Anamaliza pesa kwa kununulia mtoto nguo. Watoto wake wakati wote ni wasafi
haswa, kama Andy baba yao. Wakabaki wakimwangalia.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Akiamka
hatalia?” “Anaweza asilie. Tutaona. Sio mida yake ya kulala sasahivi.
Msingekuwa nyinyi kuwepo, angekuwa kila mahali hapa amezagaa na jina
lake likitajwa kila kona na kila mtu, akikatazwa asifanye hiki au
asishike kile. Hapo ni hofu tu inamlaza. Ataamka tu.” Raza akavuta pumzi
kwa nguvu na kuzishusha taratibu akimtizama huyo mtoto.
“Amebeba damu
nyingi ya Mina mpaka rangi si ya kina Ruhinda!” Raza akasifia na kufanya wote
wamwangalie tena pale alipokuwa amewekwa kifuani na Pius. Wakatulia kwa muda.
“Msamaha Ni
Upepo Unaofuta Vumbi, Ukiacha Njia Mpya Iangaze.”
“Jamani si mmetusamehe
kabisa?” “Yameisha Raza. Kuwa na amani.” “Nashukuru Mina, lakini acha tuombe.
Tumshukuru Mungu kwa kutusamehe mimi na familia yangu, na kuomba mwanzo
mpya wenye msingi imara wa Yesu.” Wakaona si wazo baya. Wakataka yeye
mwenyewe Raza ndio aombe. Bwana Raza aliomba mpaka akawashangaza!
Alianza kwa
kutubu akimtubia kila mmoja wao hapo kama wazazi. Alitubu Raza mpaka kwa
machozi akimsihi Mungu awasamehe pale walipokosea na kuzembea kwenye
ndoa zao na malezi ya watoto wao.
Kisha akaja kutamka
baraka kwa Mina na watoto wake mpaka Mina akafungua macho kumtizama
asiamini kama ni yeye Raza. Akamuombea Ayan uponyaji wa nafsi na fikra
akimsihi Mungu awasaidie, kumsaidia na yeye kuwa kile Mungu alichomkusudia.
Akamuombea Andy na Pius. Akaomba hekima ya Mungu juu yao wao kama wazazi
awasaidie kulea hao watoto wawe baraka kwao na kwenye jamii.
Aliomba Raza!
Ungemsikia ungejua ipo nguvu ya msalaba na Mungu ni mwingi wa rehema, na
hana upendeleo. Mpaka wanasema ‘Amen’, kila mmoja
anajisikia vizuri. Na kujiona ni wazazi wenye jukumu moja.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa watoto si
mkawalete ili tule pamoja?” Andy akatoa wazo. “Na mnaweza kuwaacha hapa walale
nyinyi mkaenda kupata muda wenu huko hotelini. Polla aje afanye fujo zake hapa,
aungane na Ayvin kwa siku hizi mbili. Watuchangamshe ndio muondoke nao.” Mina
akaongezea kwa mumewe. Pius na mkewe wakaona si wazo baya. Japo yeye Raza ndio alifurahi
zaidi kuona Polla wake na yeye hapo anakaribishwa kwa upendo na si kama
kwa shangazi yake alipofungiwa milango.
Wala hakufikiria
mara mbili, Raza mwenyewe akarudi hotelini kwa binti zake. Pius alikuwa hataki
hata kumuachia mwanae. Alibaki amemkumbatia, amejituliza kwenye kochi
hataki hata kujitingisha akihofia asije muamsha, akaondoka hapo mikononi mwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Lakini baada ya
muda mfupu akaamka na kufungua macho akiwa amesimamisha kichwa. Pius akamtizama
kwa upendo. Mina akamfanyia ishara Andy anyamaze kabisa kisha Mina akajifunika
na mto hapohapo kwenye kochi. Akabaki akimtizama Pius kisha akageuka.
Alipomuona Andy amekaa kochi la mbali kidogo akaanza kukunja kamdomo akionekana
anataka kulia. Kisha akanyoosha mikono akitaka Andy amchukue. Pius aliumia
sana mpaka alionyesha.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea….